Viongozi wateule wa Serikali za Mitaa Wilayani Geita, wametakiwa kuweka mbele maslahi ya Kitaifa kwa kuhakikisha waisimamia kwa uweledi na uaminifu miradi ambayo inatekelezwa na Serikali pamoja na kuwatumikia wananchi bila kujali tofauti zao za kisiasa.
Akizungumza hapo jana kwenye hafla ya Uapisho wa viongozi wa nyanja tofauti za Serikali za Mitaa wakiwamo Wenyekiti wa Mitaa, Vitongoji, Vijiji, pamoja na Wajumbe kutoka Kata za Katoro, Nyamigota, Ludete, Kaseme, pamoja na Magenge, katika ofisi za Kata, Katoro pamoja na Shule ya Sekondari Magenge Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Halmashauri ya Wilaya Geita, Bw. Abdallah Mkumbo, amesema kuwa Uongozi ni dhamana na hivyo viongozi ngazi ya kata wanapaswa kuwajibika na kufanya kazi kwa kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa na serikali, kwa manufaa ya wananchi, na taifa kwa ujumla.
“Mnapaswa kufahamu kuwa nafasi mlizozipata ni dhamana kutoka kwa wananchi ambao wamewaamini na hivyo mnapaswa kuwatumikia kwa uweledi bila kujali itikadi zao. Miradi inaendelea kutekelezwa kwahiyo mnapaswa kuisimamia kwa uadilifu mkubwa ili iweze kuwa na tija kwa wananchi.” Amesema Bw. Mkumbo.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Wilaya, Bw. Abdallah Mkumbo amewataka Wenyekiti wa Mitaa, Vitongoji, Vijiji, pamoja na Wajumbe kuhakikisha wanasimamia miradi inayotekelezwa na serikali kwa uadilifu na maslahi ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, Hakimu Mkazi kutoka Mahakama ya Mwanzo Katoro, Wakili Adam W. Mashiba, amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu na kuyaishi yale waliyoyatamka kwenye viapo vyao.
“Hakikisheni mnafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu zilizowekwa katika utumishi wenu kwa wananchi. Viapo vyenu vina maana kubwa na hivyo mnatakiwa mvitekeleze kwa vitendo mkizingatia Utii, Uadilifu na kutunza siri.” Amesema Wakili Mashiba.
Hakimu Mkazi kutoka Mahakama ya Mwanzo Katoro, Wakili Adam W. Mashiba akitoa maelekezo kwa Wenyetiki wateule wa Mitaa kutoka Kata za Katoro, Nyamigota, Ludete, Kaseme, na Magenge ya namna ya ujazaji wa fomu za viapo.
Aidha, kwa upande wa viongozi, Bw. Mussa William Kaniki aliyeshinda kiti cha Uwenyekiti wa Kilimahewa, Kata ya Ludete kwa tiketi ya CCM amesema kuwa atahakikisha anawahudumia wananchi na kuwatetea kwa usawa pasi na kujali tofauti zao za kisiasa, huku akitoa pongezi kwa namna zoezi zima la uchaguzi lilivyoendeshwa.
Baadhi ya Wenyekiti wa Mitaa, Vitongoji, Vijiji, pamoja na Wajumbe kutoka Kata za Katoro, Nyamigota, Ludete, Kaseme, na Magenge wakila kiapo cha Uaminifu, Utii, pamoja na Kutunza siri, mbele ya Hakimu Mkazi kutoka Mahakama ya Mwanzo Katoro, Wakili Adam W. Mashiba katika ofisi za Kata, Katoro na Shule ya Sekondari Magenge.
Zaidi ya viongozi 100 kutoka kata za Katoro, Nyamigota, Ludete, Kaseme, na Magenge walikula kiapo hapo jana kutokana na uchaguzi wa Serikaliza Mitaa uliofanyika mnamo tarehe 27, Novemba, 2024.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa