Geita
VIONGOZI wa umma Mkoani Geita wametakiwa kuwa waadilifu katika Utumishi wao ili kuendelea kuweka imani kwa wananchi katika maeneo yao ya kiutawala.
Hayo yameelezwa leo Machi 6,2025 katika Kikao Kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela akifungua mafunzo ya Maadili kwa Viongozi na Watumishi wa Umma Katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Awali akifungua mafunzo hayo yaliyoendeshwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela ameipongeza Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuendelea kufanya maboresho ya mifumo ambayo inapelekea kuwa na wepesi kwa viongozi wa umma katika utendaji na utoaji wa taarifa.
Aidha Mhe Shigela ametoa pongezi na kuwashukuru Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Geita kwa utendaji kazi wao uliopelekea kupunguza malalamiko kwa wananchi katika maeneo yao huku akiwasihi viongozi hao kuzingatia mafunzo hayo muhimu.
Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi na Watumishi wa umma Kanda ya Ziwa Ndg Godson Kweka akizungumza katika Mafunzo ya Maadili kwa Viongozi wa umma Mkoani Geita
Akizungumza katika Mafunzo hayo Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi na Watumishi wa umma Kanda ya Ziwa Ndg Godson Kweka amesema lengo la Mafunzo hayo ni kuendelea kuwakumbusha viongozi mambo ya Msingi ya Maadili ambayo wanatakiwa kuyatekeleza kwa kuzingatia sheria za Maadili.
Mwezeshaji Kutoka Ofisi ya Maadili, Kanda ya Ziwa Wakili Msomi Abigael Majige akitoa mada ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika Mafunzo yaliyofanyika Katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Kwa upande wake Mwezeshaji Kutoka Ofisi ya Maadili, Kanda ya Ziwa Wakili Msomi Abigael Majige amewataka viongozi hao kuzingatia Uadilifu katika Utendaji wao kwa kuwa ndio nguzo katika kuwaletea wananchi Maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Rajab Magaro(Kulia aliyevaa miwani) akifuatilia mada Katika Mafunzo ya Maadili kwa Viongozi wa umma katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita
"Maamuzi mnayoyafanya yana athari kubwa kwa wananchi hivyo tuzingatie maadili katika kufanya maamuzi kwa kuzingatia ukweli na uadilifu" Amesema Majige.
Pamoja na hayo Wakili Majige amewakumbusha viongozi hao kuwa wa wazi katika kutoa tamko la Rasilimali na madeni.
Vilevile wametakiwa kuwa na mwenendo mzuri wenye tabia nzuri kwa kuepuka matumizi mabaya ya madaraka.
" Tutumie dhamana tulizopewa tukijua vyeo tulivyo navyo ni dhamana ili tuweze kuwahudumia wananchi waweze kuwa na imani na Serikali yao" Ameongeza Wakili Majige.
Halikadhalika Viongozi wa Umma wametakiwa kufanya maamuzi kwa kuzingatia misingi ya sheria, kanuni na taratibu pasipo upendeleo katika kutoa huduma kwa kuwa na lugha nzuri kwa wananchi kuondoa mgongano wa maslahi.
Viongozi mbalimbali wa Umma Mkoani Geita wakiwa Katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita katika Mafunzo ya Maadili kwa Viongozi wa umma
Mafunzo hayo wamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwepo Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Geita, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya, Viongozi wa Ulinzi na Usalama na Wakuu wa Idara na Vitengo katika Halmashauri za Mkoa wa Geita.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa