Nzera-Geita
VIONGOZI wa Serikali za Mitaa na Watumishi Viongozi Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Februari 4,2025 wamepewa mafunzo ya Uraia na utawala bora ili kuwajengea uelewa mpana katika Utekelezaji wa Majukumu yao.
Awali akifungua Mafunzo hayo kwa Niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Komba, Katibu Tawala wilaya ya Geita Bi Lucy Beda amewataka viongozi hao kupeleka maarifa na ujuzi kuanzia ngazi ya familia na maeneo ya kazi.
Katibu Tawala Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda akizungumza katika Mafunzo ya Elimu ya uraia na utawala bora katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita-Nzera
"Ninafahamu kuwa wote mnaoshiriki mafunzo haya mnawakilisha kundi kubwa la watumishi walio chini yenu, hivyo Niwaombe msiwe wachoyo, pelekeni elimu mtakayoipata katika mafunzo haya kwa watumishi wengine" Amesema Bi Lucy Beda.
Aidha Katibu Tawala huyo ameongeza kwa kusema mafunzo hayo yamefanyika wakati muafaka kwa kuwa Wilaya ya Geita kumekuwepo changamoto katika Utekelezaji wa haki za Binadamu.
Pamoja na hayo Bi Lucy Beda ametoa rai kwa viongozi hao kwenda kuyatumia mafunzo waliyopatiwa kama chachu ya kuleta mabadiliko katika usimamizi ulinzi wa haki za Binadamu na misingi ya utawala bora ili kukuza Demokrasia na kudumisha amani na utulivu katika Wilaya ya Geita na Nchi kwa ujumla wake.
Akizungumza katika Mafunzo hayo Mratibu wa Mafunzo Mhe Joyce Mushi ambaye ni Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria amesema Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuwezesha utatuzi wa Migogoro mbalimbali kwa kuendelea kutoa elimu ya masuala ya uraia na utawala bora kwa viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa.
" Wizara ya Katiba na Sheria ni moja ya vinara wa utekelezaji wa 4Rs ambazo ni Maridhiano( Reconciliation) Ustahimilivu ( Resilience) Mabadiliko ( Reforms) na Kujenga upya (Reconstruction)" Amesema Mhe Joyce Mushi.
Aidha Wakili Mushi amesema lengo la Wizara ya Katiba na Sheria kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo viongozi ili waweze kutekeleza majukumu yao pasipo kuvunja sheria, vilevile kuendelea kuwajengea viongozi uwezo wa masuala ya haki na wajibu, demokrasia na utawala bora, madaraka ya umma na ulinzi na usalama.
Vilevile Wakili huyo ameongeza kwa kusema kupitia mafunzo hayo viongozi wataendelea kupata uelewa kukuza na kuendeleza uzalendo na utaifa, na kuweza kujua namna ambavyo wanaweza kushughulikia malalamiko ya wananchi katika ngazi zao za utawala kwa ufanisi na ueledi.
Pamoja na hayo Wakili Mushi amewataka Viongozi hao kupitia elimu waliyopata kuifikisha katika ngazi au viongozi walio chini yao wakiwemo wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji.
Halikadhika Viongozi hao wametakiwa kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini kwa kufuata Misingi ya Demokrasia na Utawala bora.
Mafunzo hayo ya elimu ya uraia na utawala bora yametolea katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita-Nzera ambapo mada mbalimbali zimewezeshwa katika mafunzo hayo ikiwemo mada ya Demokrasia na Utawala bora, Haki na Wajibu, Ulinzi na Usalama pamoja na Madaraka kwa umma.
Watendaji wa kata Wakiwa katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita-Nzera ambapo wamejifunza elimu ya uraia na utawala bora
Mafunzo hayo yametolewa na Wataalam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora na Jeshi la Polisi ambapo walengwa katika mafunzo hayo walikuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama, baadhi ya wakuu wa divisheni za Halmashauri na watendaji wa kata.
Mafunzo ya Elimu ya uraia na utawala bora yamekwishatolewa katika Mikoa mitano kwa awamu ya kwanza na sasa ni awamu ya pili inaendelea kutolewa katika mikoa 6 hivyo kupelekea jumla ya mikoa 11 ambayo ni Rukwa, Mara, Songwe, Uringa, Morogoro, Kigoma,Geita Katavi,Katavi, Tabora, Mtwara na Kilimanjaro
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa