Jmla ya Shilingi Milioni 893, ikiwa ni fedha kutoka mfuko wa Serikali Kuu pamoja na fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), zimetumka kuchangia ujenzi wa wodi mpya tatu katika Hospitali ya Wilaya, Geita, iliyopo Kata ya Nzera.

Hatua hii muhimu imeweza kufikiwa ikiwa ni juhudi za Serikali katika kutatua kero za wananchi hususani katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu mbali mbali pamoja na kupunguza idadi ya vifo haswa kwa kundi la akina mama na watoto wakati wa kujifungua.

Akizungumza tarehe 6, Agosti kwenye ziara ya Ukaguzi wa Miradi pamoja na njia itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba ameipongeza timu ya menejimenti ya Hospitali hiyo kwa kusimamia ujenzi wa wodi hizo za kisasa huku akiitaka iongeze msukumo kwenye eneo la utunzaji wa miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu.

Mradi huo ambao unatarajiwa kuzinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwanzoni mwa Mwezi Septemba, utakuwa na faida mbali mbali ambapo utasaidia katika kutatua changamoto ya msongamano kwenye Hospitali hiyo, huku pia ukipunguza uwezekano wa kutokea magonjwa ya kuambukizwa.

Huduma za afya zimekuwa ni kipaumbele kikuu na hivyo Serikali imeendelea na juhudi za kuhakikisha inaboresha miundombinu ili wananchi waweze kuwa na afya bora na salama.

Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa