Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Halmashauri ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Magaro mapema leo Novemba 27, 2024 amepiga kura katika Kata ya Nzera yalipo makao makuu ya Halmashauri.
Akiwa katika kata ya Nzera, Magaro ameendelea kutoa hamasa kwa wananchi wengine kujitokeza siku ya leo ili kutimiza haki yao ya Kidemokrasia katika uchaguzi huu wa serikali za Mitaa.
Wananchi wakiwa katika foleni kuelekea kwenye chumba cha kupiga kura katika kijiji cha Nzera Kata ya Nzera. Vituo vya upigaji kura vimefunguliwa mapema saa mbili na mamia ya wananchi wameendelea kujitokeza kutimiza haki yao ya Kidemokrasia
“Nimeshiriki katika kuchagua viongozi wa serikali za mitaa katika kijiji ninachoishi Nzera, nipende kutoa hamasa kwa wananchi kutumia haki yao ya Kidemokrasia kuchagua viongozi katika maeneo yao waliyojiandikisha.” Amesema Magaro.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Magaro akipiga kura mapema leo asubuhi katika Kata ya Nzera alipojiandikisha.
Pamoja na kupiga Kura, Ndg Magaro ametembelea vituo mbalimbali ndani ya Halmashauri vya kupiga kura ili kujionea zoezi hilo linavyoenda.
Vilevile akiwa katika vituo hivyo Ndg Magaro ameishukuru Serikali inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka maandalizi mazuri katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili wananchi waweze kushiriki uchaguzi katika mazingira mazuri.
Wananchi wakiwa katika kituo cha kupiga kura kuangalia majina yao kabla ya kupiga kura mapema leo Novemba 27,2024
Upiga wa kura umeanza mapema leo saa mbili asubuhi ambapo vituo vilikuwa wazi na mamia ya wananchi wameendelea kujitokeza katika upigaji kura ambapo zoezi hilo linatarajiwa kukamilika majira ya saa kumi jioni.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina majimbo mawili ya Uchaguzi yenye Kata 37, Vijiji 145 na Vitongoji 593 ambapo jumla ya vyama 7 vya Siasa ambavyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Demokrasia na Maendelo(CHADEMA), ACT WAZALENDO, CCK, TLP na ADC vinashiriki Uchaguzi huo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa