Timu ya Uratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, 2025 (M) Geita, imetembelea na kukagua njia pamoja na miradi itakayotembelewa na Mwenge huo, na kuridhishwa na hatua ya ukamilishaji iliyofikiwa mpaka sasa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala (M) tarehe 7 Agosti, wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa timu hiyo, Ndg. Abdallah Mkumbo amesema kuwa hatua iliyofikiwa na Halmashauri kwenye miradi hiyo, ni ya kuridhisha, huku pia akitoa maelekezo kwa Wakuu wa Idara wenye miradi kuhakikisha hati pamoja na nyaraka muhimu za miradi hiyo, zinawekwa vizuri.

Ndg. Mkumbo pia amewataka wahandisi kuhakikisha wanawasimamia mafundi ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa ubora unaotakiwa.

Kwa upande wa mradi wa Shule mpya ya mkondo wa Amali, Sekondari ya Chibingo, Kata ya Nyamigota uliogharimu kiasi cha fedha, Milioni 584.2, timu hiyo ilikagua Jengo la Utawala, Madarasa 8, Ofisi 2, Maktaba, Jengo la TEHAMA, Maabara itakayotumika kwa masomo ya Sayansi, pamoja na nyumba moja ya Mtumishi.

Mradi huo unatarajiwa kuzinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru, 2025 ambapo utafaidisha wanafunzi kwa kuwawezesha kupata maarifa na ujuzi wa nadharia sambamba na vitendo, unaohitajika kwenye soko la ajira, hivyo kuwawezesha kujitegemea na kuwa na mchango chanya kwenye taifa.

Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa