Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuwa Novemba 19, ambayo ni Siku ya Wanaume Duniani, inapaswa kutambuliwa rasmi kama ilivyo Machi 8, Siku ya Wanawake Duniani.
Akizungumza Machi 2, 2025, katika Kongamano la kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Kanda ya Ziwa lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ushirombo, Bukombe, mkoani Geita, Mhe. Gwajima alisema ushirikishwaji wa wanaume katika masuala ya jinsia ni muhimu kwa maendeleo ya wanawake na watoto wa kike.
“Wanaume mpo kisera kabisa, hivyo ni muhimu kushiriki katika mchakato wa maendeleo ya wanawake. Nitaiomba Novemba 19 iwe siku rasmi kama ilivyo Machi 8,” alisema.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na Mamia ya Wananchi waliojitokeza katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Kimkoa yaliyofanyika katika Viwanja vya Ushirombo Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita
Katika kongamano hilo, Mhe. Gwajima alitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali yaliyokuwa yakionyesha shughuli na mafanikio yao. Akiwa katika banda la Halmashauri ya Wilaya ya Geita, alifurahishwa na mafanikio ya wajasiriamali waliopata mikopo yenye riba nafuu, akiahidi kuwa mikopo hiyo itaendelea kutolewa kwa awamu ya tatu na ya nne.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela, alisema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yamefanikiwa kutekelezwa, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi. Kati ya majukwaa 549 yaliyopangwa, tayari 539 yameanzishwa, huku mengine 10 yakiwa mbioni kukamilika.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela akizungumza Katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Kimkoa yaliyofanyika Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita Machi 2, 2025
Aidha, Mhe. Shigela alieleza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 1.5 zimetolewa kwa vikundi 173 vya wanawake, huku vikundi 63 kati ya hivyo vikiwa vya wachimbaji wa madini, hatua inayoongeza tija kwa shughuli za kiuchumi za wanawake. Pia alizitaka taasisi za fedha kuendelea kupunguza riba kwa wanawake wanaohitaji mikopo.
Katika hotuba yake, Mhe. Gwajima alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa mikopo rafiki kwa wanawake na itaendelea kuhakikisha kuwa riba inakuwa nafuu ili kuwainua kiuchumi.
Baadhi ya Matukio katika Picha Siku ya Maadhimisho ya siku ya Wanawake Mkoani Geita ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa