Walengwa wa mpango wa Serikali wa kunusuru kaya masikini TASAF watakiwa kuwapeleka watoto shule na kufuatilia maendeleo yao ili waweze kuwa na sifa za kusaidiwa na mpango huo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Geita Josephat Maganga wakati akiwa kwenye ziara ya kukutana na kuzungumza na walengwa wa TASAF katika vijiji vya Wigo na Ililika vilivyopo Halmashauri ya Wilaya Geita.
Alisema Serikali kupitia mpango wa kusaidia kaya masikini inasomesha watoto wa walengwa waliopo shuleni pia kuwapa fedha za malezi watoto wenye umri kuanzia miaka 0-5 ambao wanapelekwa kliniki.
Aidha Maganga amewapongeza waratibu wa TASAF kwa kuwalipa walengwa fedha kulingana na misingi pamoja na taratibu za mpango huo, pia amewataka kuendelea kuwapa elimu na kuwakumbusha staiki zao.
Kwa upande wake mratibu wa TASAF mkoa wa Geita Elikana Haroun amesema Serikali inawataka walengwa wa TASAF kutumia fedha hizo vizuri ili kujikwamua katika janga la umaskini hivyo waendelee kutumia fedha hizo kuanzisha miradi midogo midogo.
Nae mratibu wa TASAF wilaya ya Geita Gabriel Evarist, amesema kabla ya mpango wa TASAF kuwafikia walengwa hali zao za kimaisha zilikuwa duni lakini kwa sasa kumekuwa na aueni kwa sababu wanatumia fedha wanazozipata kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Mtendaji wa kijiji cha Wigo Marco Kimanyo ameishukuru Serikali kwa kuleta mpango huo wa kunusuru kaya maskini kwani walengwa wamefanikiwa kujiunga katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama ufugaji, kilimo na biashara ndogondogo pamoja na kuboresha makazi yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa