Na. Michael Kashinde
Shirika la SEDIT linaloshirikiana na PLAN International pamoja na Kivulini katika kutekeleza mradi wa kutokomeza ajira hatarishi na ukatili kwa watoto awamu ya Tatu mwaka 2020 - 2023 limegawa vifaa mbalimbali zikiwemo mashine za nafaka kwa vikundi mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ikiwa ni mwendelezo wa harakati zake za kuchochea ukuaji wa kipato kuanzia ngazi ya familia.
Agosti 15, 2022 shirika hilo linalofanya kazi katika kata nne za Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambazo ni Nyamigota, Magenge, Nkome na Senga zenye jumla ya vijiji 15 limevifikia vikundi linavyovilea na kuvipatia vifaa hivyo kulingana na mahitaji ya vikundi husika.
Aidha vikundi vilivyofaidika na mgawo huo ni pamoja na Amani kutoka Senga waliopata mashine ya kupukuchua mahindi, Upendo kutoka Senga wakipatiwa mashine ya kusaga mahindi huku kikundi cha Amani kutoka Nkome kikipatiwa mashine ya kusaga karanga na siagi ya karanga.
Vikundi vingine ni pamoja na Vijana shupavu kutoka Senga waliopatiwa Seti ya vifaa vya kulishia kuku, Wajasiriamali makatani kutoka Nkome waliopatiwa Incubator, Nyikonga Magenge na Mabinti Shujaa kutoka Nyamigota waliopatiwa vyerehani viwili viwili kwa kila kikundi.
Vifaa vingine ilivyotolewa na Shirika la SEDIT ni pamoja na Embroider Machine, Grinder, pampu ya maji, mpira wa maji, na Mashine ya kufyatulia tofali huku thamani ya vifaa vyote vilivyotolewa ikiwa ni Tshs.14,878,500/= ambapo kati ya hizo kiasi cha Tshs. 12,944,700/= zimetolewa na mradi huku Tshs. 1,933,800/= zikichangwa na vikundi vitatu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.
Bw.Thoba John Mratibu wa mradi wa Utokomezaji wa ajira hatarishi na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto awamu ya tatu akizungumza wakati wa kukabidhi baadhi ya vifaa hivyo katika kata ya Senga amesema kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuna jumla ya vikundi 58 ambapo vikundi 12 vimepewa vifaa na mashine hizo ili kuungwa mkono kutokana na ubunifu na juhudi zao katika miradi mbalimbali ya vikundi kulingana na maeneo yao.
Aidha Bw. Thoba ameendelea kwa kusema kuwa kupitia vikundi hiyo vya hisa mradi umeweza kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali kupitia wawezeshaji jamii na kuwawezesha wanachama kuanzisha miradi ya mtu mmoja mmoja na pia imeanzishwa miradi mbalimbali ya vikundi ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mazao, ulimaji bustani, ufyatuaji wa tofali, useremala, ufugaji wa kuku,ushonaji wa nguo na miradi mingine.
Kwa upande wake Afisa Maendeleleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bw. Novatus Bituro amewasihi wanavikundi waliopokea vifaa hivyo kuvitunza, kuvithamini na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa huku akisisitiza kuwa ana Imani vifaa hivyo vikitumiwa kama inavyotakiwa vitakuwa chachu ya kukua kwa miradi ya walengwa kwa kuwa watajipatia kipato cha uhakika kitakachosaidia kukuza uchumi wa kaya zao.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa