Nzera-Geita.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Rajab Magaro amelieleza baraza la Madiwani katika Mkutano wa kawaida wa robo ya pili kuwa Halmashauri imepanga kutoa Mikopo yenye thamani ya Shilingi Milioni 850.
Magaro amesema mikopo hiyo ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ambapo hadi sasa jumla ya vikundi 187 vimeomba mikopo hiyo huku vikundi vya wanawake vikiwa 94, vijana 92 na watu wenye ulemavu 16.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda, ameipongeza Halmashauri kwa kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kutoa mikopo ya vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.
“Niipongeze Halmashauri kwa kutumia mapato yake ya ndani asilimia 10 ili kuwawezesha wananchi kiuchumi” Amesema Bi.Beda.
Pamoja na hayo Katibu Tawala kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Komba ametoa wito kwa Madiwani kuendelea kuweka udhibiti katika ukusanyaji wa mapato ili kufikia lengo na kulivuka ambapo ameongeza ili hayo yafanyike Halmashauri inapaswa kuendelea kuwa na utulivu ili kuweza kufanya kazi zake vizuri.
Mikopo hiyo inatarajiwa kutolewa maara baada ya ukaguzi wa miradi ya vikundi ngazi ya kamati ya uhakiki wa mikopo ngazi ya Wilaya kukamilika ambapo vikundi vitakavyokuwa vimekidhi vigezo vitanufaika na Mikopo hiyo.
Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2024/25 imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 1.8 kwa vikundi 111 na kwa mwaka 2025/26 tayari kiasi cha Shilingi Milioni 500 kimekwisha kutolewa kwa vikundi 58.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa