Mkuu wa Wilaya ya Geita Wilson Shimo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyowawezesha wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo suala linalosaidia kukuza uchumi.
Ameyasema hayo katika maonesho ya nne ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini katika viwanja vya bombambili alipotembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kujionea bidhaa mbalimbali zilizoandaliwa na Wajasiriamali wa Wilaya hiyo.
Amesema kuwa mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa ajili ya wanawake,vijana na walemavu imekuwa msaada mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi huku akiwashauri wajasiriamali kuendelea kutengeneza bidhaa zinazohitajika kwa wingi ikiwemo mafuta ya kupikia.
kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita amewapongeza wajasiriamali hao kwa kazi nzuri wanazozifanya huku akiwataka kuendelea kuwaelimisha zaidi wananchi wanaotembelea banda hilo kuangalia bidhaa hizo.
Aidha ameendelea kueleza kuwa bidhaa zote zinazoonekana katika banda hilo la Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni kiashiria cha shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika Halmashauri hiyo ikiwemo uchimbaji wa Dhahabu ambao unafanyika katika kata 10 za Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Maonesho hayo yameanza septemba 16 mwaka huu yakiratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, ambapo kilele chake ni septemba 26 na Mgeni Rasmi akiwa Waziri mkuu wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa anayetarajiwa kufika viwanjani hapo septemba 22,huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ’’SEKTA YA MADINI KWA UKUAJI WA UCHUMI NA MAENDELEO YA WATU”
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa