Nzera-Geita
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa vifaa mbalimbali vya kufundishia na kujikimu kwa walimu wa shule za msingi wenye ulemavu wa viungo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa walimu saba (7) wanaofundisha katika shule tofauti za msingi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ambapo miongoni mwao wapo walimu wenye ulemavu wa viungo na ulemavu wa ngozi
Akizungumza wakati wa makabidhiano Februari 2, 2026 iliyofanyika katika ofisi za Halmashauri-Nzera, Mwakilishi wa serikali ambaye ni Afisa Elimu Maalum , Mwl Shiku Jackson alisema kuwa utoaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya mkakati wa Wizara wa kuhakikisha usawa, ujumuishi na mazingira rafiki ya kazi kwa walimu wenye mahitaji maalum.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mafuta ya kujipaka 37 kwa ajili ya walimu wenye ulemavu wa ngozi, kofia 1, kifaa kimoja cha kurekodia sauti, Kompyuta mpakato 2 pamoja na vishikwambi 4, ambavyo vitawasaidia walimu hao katika ufundishaji na maandalizi ya masomo.
Kwa upande wao, walimu waliopokea vifaa hivyo wameishukuru serikali kwa kuwajali na kuwatambua, wakisema msaada huo utaongeza ari, ufanisi kazini na kuboresha utoaji wa elimu kwa wanafunzi.
Serikali imeendelea kusisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha walimu wote, hususani wenye mahitaji maalum, wanapata mazingira bora ya kazi na haki sawa katika sekta ya elimu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa