Na: Hendrick Msangi
Wakala wa maji safi na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) wilayani Geita katika taarifa yake kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika May 9, 2024 makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeazimia kupunguza magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama kama vile kuhara, homa ya matumbo na Kipindupindu.
Hayo yameelezwa katika Kikao cha baraza la madiwani wakati wa uwasilishaji wa utekelezaji wa shughuli za serikali ngazi ya Halmashauri na taasisi kwa kipindi cha robo ya tatu Januari hadi Machi 2024 ambapo katika taarifa yake, Injinia Sande Batakanwa ambaye ni Meneja Ruwasa Wilayani Geita imesema Ruwasa pamoja na kupunguza magonjwa hayo pia upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mengi ndani ya Halmashauri umeokoa muda uliokuwa unatumika kufuata maji mbali na kupelekea kusimama kwa shughuli nyingine za uzalishaji.
Baadhi ya Madiwani katika kikao Cha baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakifuatilia Kwa umakini nyaraka za taarifa za Utekelezaji wa Shughuli za Maendeleo yaliyotekelezwa Kwa kipindi Cha Januari hadi Machi mwaka huu 2024.
Utekelezaji wa miradi hii umeendelea kutoa ajira kwa vijana wengi ndani ya Halmashauri ambapo Ruwasa imekuwa ikitumia nguvu kazi iliyopo maeneo miradi inapotekelezwa na kufungua fursa za kiuchumi.
Jumla ya kata 5 ambazo ni Nkome, Katoma, Nyamboge, Nzera na Lwezera zinapata maji safi na salama kutokana na maboresho yanayoendelea kufanyika na Wakala wa maji safi na Usafi wa mazingira (RUWASA)
Huduma ya maji vijijini kwa Wilaya ya Geita inapatikana kupitia vyanzo mbalimbali vya maji vikiwemo visima vifupi (83) visima virefu (140) maji ya bomba toka Ziwa Viktoria na visima vya asili 130.
Wilaya ya Geita ina miradi ya mtandao 21 katika meneo mbalimbali ndani ya wilaya ambayo inatoa huduma za maji kwenye vijiji 26 na miradi ya pampu 148 inayotoa huduma kwenye vijiji 75. Miradi ya myandao ni pamoja na Chankorongo, Izumacheli, Mharamba, Nyamboge, Nzera,Nyakagomba, Luhula, Inyara, Njiapanda Inyara, Kasesa, Kaseme, Lwamgasa, Nyakagwe, Kamena, Ikina, Nyamalimbe, Katoma, Mawemiru, Nkome, Busanda na Katoro.
Katika taarifa hiyo, imeeleza jumla ya kiasi cha shilingi 1,881,029,138.40 zimepokelewa kwa ajili ya miradi ya maji huku fedha iliyotengwa katika bajeti ya mwaka 2023/2024 ni kiasi cha shilingi 3,240,232,481.13.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuleta fedha nyingi ili kutimiza dhamira yake ya kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana katika kila kijiji ikiwa ni utekelezaji wa kampeni yake ya kumtua mama ndoo kichwani.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa