Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kupata hati safi katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali CAG kwa mwaka wa Fedha 2021/2022.
Ametoa Kauli hiyo akiwa kama mwenyekiti katika kikao cha Baraza maalumu la madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita kilichokaa Juni 23, 2022 katika ukumbi wa Halmashauri Nzera kwa ajili ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali CAG.
Mhe. Senyamule amesema Halmashauri zote za Mkoa wa Geita zimefanya vizuri na kupata hati safi hali inayoupa heshima Mkoa wa Geita, huku akiipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kukusanya mapato mengi zaidi ya makadirio ya bajeti.
Aidha Mhe. Senyamule amewataka viongozi mbalimbali kuongeza juhudi na maarifa katika kusimamia miradi mbalimbali ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa ili Kuendelea kumtia Moyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ndani ya Mkoa wa Geita.
Wakati huo huo Mhe. Senyamule ametumia nafasi hiyo kuwataka viongozi mbalimbali kusimamia suala la upatikanaji wa chakula mashuleni na kudhibiti utoro, huku akitoa wito kwa viongozi kuwahamasisha wananchi kushiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi bila kusahau kuyatangaza maendeleo yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo akizungumza katika kikao hicho amewataka wakaguzi wa ndani kushirikiana na wakuu wa Idara mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili awamu ijayo wapunguze hoja.
Wakati huo huo Mkaguzi Mkuu wa nje Mkoa wa Geita CPA Richson Ringo akizungumzia taarifa ya hoja hizo amewashauri Wakuu wa Idara na watumishi wote kwa ujumla kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu za manunuzi ili kuepuka hoja, huku akiwataka idara ya manunuzi kuwa na kumbuumbu ya nyaraka zote zinazotakiwa katika manunuzi.
Katika kikao hicho cha Baraza maalumu la Madiwani Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg. John Paul Wanga alianza kwa kuwasilisha hoja zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Charles Kazungu akizungumza katika kikao hicho amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita itafanya hima kuhakikisha inazifuta hoja za mkaguzi, huku akishauri kutolewa kwa fedha za kutosha katika mikopo ya makundi maalumu ili fedha hizo ziwe na tija kwa wanufaika.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa