Nzera-Geita
Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetoa kiasi cha Shilingi Milioni 689,000,000 ikiwa ni sehemu ya asilimia 10 ya mikopo inayotolewa na Serikali kwa makundi ya watu wenye ulemavu, vijana na wanawake.
Akizungumza katika Hafla ya uzinduzi wa utoaji wa mikopo na vitambulisho vya wajasiliamali katika viwanja vya Halmashauri-Nzera, Februari 10, 2025, Katibu Tawala Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Komba amelipongeza Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa namna ambavyo wanaisimamia Halmashauri na kuweza kutenga fedha hizo ili wananchi waendelee kunufaika.
Katibu Tawala Wilaya ya Geita Bi Lucy Beda akizungumza katika hafla ya ugawaji mikopo Halmashauri ya Wilaya ya Geita
“Kwa namna ya kipekee tumshukuru Rais wetu Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kurejesha mikopo kwa upendo wake na mapenzi makubwa aliyo nayo kwa Watanzania ili waweze kujikwamua kiuchumi.” Amesema Bi Lucy Beda.
Aidha Katibu Tawala huyo amewaasa wana vikundi wote walionufaika na mikopo hiyo kuendelea kuimarisha mahusiano kwenye vikundi na kuepuka migogoro ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea katika vikundi hivyo.
“Tujiepushe na migogoro, tuendelee kushikamana ili malengo ya mikopo yafikiwe na kila mmoja awe na taarifa sahihi za kikundi kujua nini kinaendelea” Amesisitiza Bi Lucy Beda.
Pamoja na hayo, Bi Lucy Beda ameongeza kwa kusema, Serikali imeviamini vikundi hivyo na kuwataka kuendelea kushikamana kwani Serikali imetoa mikopo isiyo na riba na kuwataka kufanya kazi kwa bidii ili waweze kurejesha fedha walizokopeshwa na kuepuka kuitumia mikopo hiyo kwenda maeneo mengine kukopa.
Vile vile Katibu Tawala huyo amewasihi wana vikundi hao kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili na wananchi wengine wenye sifa waweze kupata mikopo hiyo isiyokuwa na riba huku akisisitiza kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha Beda ametoa rai kwa Maafisa Maendeleo kwa ngazi ya kata kuvitembelea vikundi vilivyokopeshwa mara kwa mara ili kujua changamoto zozote wanazokutana nazo na kuzitatua kwa wakati na kuendelea kutoa elimu kwa ambao hawajapata mikopo hiyo ili waweze kuomba mikopo ya Serikali isiyokuwa na riba katika kutimiza adhma ya Dkt Samia ya kuwahudumia wananchi.
Itakumbukwa kuwa Serikali ilisitisha zoezi la utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Aprili 2023 kutokana na sababu mbalimbali zikiwepo namna ya uratibu wake na urejeshwaji wa mikopo hiyo na baadaye Septemba 2024 Serikali ilikamilisha uandaaji wa kanuni mpya na kuruhusu Mamlaka za Serikali za mitaa kuendelea na zoezi la kutoa mikopo.
Baadhi ya pikipiki ambazo zimetolewa mkopo kwa kundi la Vijana maarufu kama bodaboda
Kwa upande wake Ndg George Kitaba ambaye ni mnufaika wa mikopo hiyo kutoka kundi la Walemavu ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe DKT Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha mikopo hiyo. “ Kikundi chetu cha Walemavu Msasa-Busanda ni mara ya tatu kuchukua mkopo tulianza na milioni 6 na sasa tumepewa Milioni 20” Ameongea kwa furaha ndg George Kitaba.
Naye Bi Magdalena Andrea mwanakikundi kutoka Wanawake na Mendeleo –Kasota ambacho kinajishughulisha na shughuli za ufugaji ameishukuru Serikali kwa kutoa mikopo hiyo ambayo inawasaidia kuanzia ngazi ya familia na kusema kikindi hicho kimepokea kiasi cha Shilingi Milioni 20 ukiwa ni mkopo wao wa 5 tangu wameanza kukopa katika Halmashauri.
Jumla ya Vikundi 39 kati ya 47 vimekidhi vigezo vya kupewa mikopo hiyo ambavyo wanawake ni vikundi 23, vijana vikundi 14 na vikundi vya watu wenye ulemavu 2 ambapo kiasi cha Shilingi Milioni 689,000,000 kimetolewa katika awamu ya kwanza.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa