Halmashauri ya Wilaya ya Geita inatarajia kunufaika na mradi wa keeping Adolescent Girls in School wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 17,utakaofadhiliwa na kutekelezwa na shirika la Plan International katika kipindi cha miaka 5 kuanzia 2022.
Hayo yamezungumzwa Septemba 15, 2021 na Mkurugenzi wa mradi huo ndg.Nicodemus Gachu,alipotembelea ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Nzera.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika shule 16 za msingi na shule 3 za sekondari katika kata za Ludete ,Katoro na Nyamigota.
Lengo la mradi ni kuwasaidia watoto wa kike walio shuleni kuwajengea mazingira rafiki yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao katika maisha, nakutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kama vile mimba za utotoni pamoja na mazingira hatarishi au magumu,yanayopelekea watoto wa kike kushindwa kuendelea na masomo.
Lengo la mradi linatarajiwa kutekelezwa kwa kujenga vyoo bora vyenye miundombinu ya maji ikiwemo na vyumba vya kujisitiri wakati wa hedhi,kugawa taulo za kike kwa ajili ya dharura,kutoa vitabu vya kiada na ziada,na kutoa baiskeli kwa watoto wanaokaa mbali na maeneo ya shule.
Aidha malengo mengine ni pamoja na kutoa vifaa vya shule kwa watoto walio katika mazingira magumu kwa kutumia utaratibu wa vocha kama vile madaftari,kalamu na mabegi,kutoa elimu isiyo rasmi kwa watoto walio chini ya mfumo rasmi kama vile kuepuka mimba za utotoni na utengenezaji wa taulo za kike lakini pia kutoa mafunzo kwa wadhibiti ubora wa shule juu ya masuala mbalimbali yanayohusu elimu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa