Waziri wa Nishati Dokta Medard Kalemani(MB) amewataka wakandarasi wanaofanya kazi katika mradi wa umeme vijijini(REA) kutokuruka kaya yoyote ile kwa visingizio visivyo na tija ili wananchi wote wenye sifa wapate umeme kwa gharama nafuu.
akiongea na wakazi wa kijiji cha Nyamwilolelwa kata ya Nyamwilolelwa Halmashauri ya wilaya ya Geita wakati wa zoezi la uwashaji wa Umeme katika kijiji hicho amesema kwa sasa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dokta John P. Magufuli imedhamiria kwa dhati kupeleka huduma ya umeme katika vijiji vyote nchini ili kusukuma kasi ya maendeleo hasa katika kipindi hiki cha kuipeleka Tanzania kuwa ya viwanda.
Mheshimiwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani(Mb) akiwasha umeme katika kijiji cha Nyamwilolelwa kuashiria kuanza kwa huduma hiyo na zoezi hilo likishuhudiwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (aliyevaa miwani)
Aidha Dokta Kalemani amewahakikishia wakazi wa jimbo la Busanda kuwa mradi wa maji Chankolongo kutoka ziwa Viktoria muda si mrefu utaanza kufanya kazi maana sababu ilikua ni kukosa umeme wa kusukuma pampu za maji na tayari shirika la ugavi wa umeme nchini TANESCO limejipanga kupeleka mafundi kuanzia wiki ijayo.
Sambamba na hilo Dokta Kalemani amewataka wananchi kutumia vifaa vya UMETA (Umeme tayari) katika taasisi zilizopo katika vijiji vyao hasa ofisi za vijiji na Zahanati kwani ni kifaa cha bei rahisi na kinafaa kwa vyumba vichache bila kufunga mfumo wowote wa waya.
Mheshimiwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani(Mb) akimkabidhi mbunge wa jimbo la Busanda Lolensia Bukwimba kifaa cha UMETA ikiwa ni zawadi kwa wazee kumi wasiojiweza katika kijiji cha Nyamwilolelwa
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Busanda Mheshimiwa Lolensia Bukwimba amemshukuru waziri Kalemani kwa kuhakikisha vijiji 60 kati ya vijiji 89 katika awamu ya pili na ya tatu ya REA vitaunganishwa na umeme na pia vijiji 5 vitapata umeme utakaopita kutoka bulyanhulu hadi Mpomvu Geita kutakapojengwa kituo cha kupooza umeme ambacho kitatoa megawati 98 kwa Mkoa wa Geita.
Waziri Kalemanii amemaliza ziara yake ya kikazi katika wilaya ya Geita na ameelekea wilayani Chato ambako atakua na shughuli za kukagua miradi ya umeme na kuongea na wananchi wilayani humo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa