Na: Hendrick Msangi
Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba, ametoa maagizo kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo zahanati katika vijiji vinne ambavyo ni Butobela, Nyang'homang, Shahende, Nyakagwe pamoja na ujenzi wa daraja na shule ya msingi Mhande kata ya Butobela tarafa ya Busanda wilayani Geita.
Ujenzi wa Kituo cha Afya Kijiji cha Nyakagwe, wenye thamani ya shilingi milioni 200.
Maagizo hayo yametolewa Alhamisi May 16 2024, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nyakagwe kata ya Butobela, ikiwa ni mwendelezo wa Ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ndani ya halmashauri wilaya ya Geita Pamoja na kusikiliza kero za Wananchi.
Wananchi wa kata ya Butobela wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba.
Amesema Serikali pamoja na wadau ( CSR) kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na wananchi waweze kupata uhakika wa huduma za afya kupitia kituo cha afya cha Nyakagwe ambacho ujenzi wake bado unaendelea pia ukamilishwaji wa ujenzi wa daraja linalounganisha kijiji cha Butobela na Nyakagwe.
Ujenzi wa daraja la midomo miwili ya mita 2 kwa mita 4( Double Cell 2x4) barabara ya Bukoli -Nyakagwe kwa gharama ya TSH 146,235,700.00 unaotarajiwa kukamilika May 30,2024 chanzo cha fedha kikiwa ni Tozo. Mradi huo unasimamiwa na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA).
Aidha ameiagiza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuendelea kuweka msukumo wa kumalizia miradi viporo kwa kuendelea kuipa kipaumbele katika bajeti za CSR na mapato ya ndani.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ndg Karia Rajabu Magaro amewapongeza Wananchi wa Kata ya Butobela kwa kupenda Maendeleo na kuanzisha Miradi ya Maendeleo na kusema wajibu wa Serikali ni kuhakikisha kuna kuwa na Mipango endelevu ya ukamilishaji wa Miradi.
"Fedha zinapokuja muwe walinzi wa fedha hizo ili zikidhi malengo yaliyo kusudiwa na Wananchi wapate taarifa ya mapato na matumizi ikiwa ni pamoja na Kamati za ujenzi zinakuwa pamoja kusimamia ujenzi wa mradi ili vifaa vinavyoletwa vitumike ilivyokusudiwa" amesema Karia.
Akiendelea kuzungumza na Wananchi wa kata ya Butobela, Mh Komba amesema kero kuu katika kata hiyo ni barabara kwani itawasaidia wananchi kutoka katika vijiji ambavyo havina zahanati ndani ya kata hiyo kuweza kupata huduma za afya katika kituo cha afya cha Nyakagwe na kuwaomba wawekezaji na wachimbaji wa Madini katika kata hiyo kupitia fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) kusaidia kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa barabara.
Pamoja na hayo wananchi wa kata ya Butobela wametoa kero zao katika mkutano huo ambapo changamoto kubwa ni upatikanaji wa huduma za afya, uhaba wa umeme katika baadhi ya vitongoji hasa maeneo yenye Shughuli za uchimbaji wa madini, uhaba wa walimu katika shule ya msingi Nyakagwe, na ubovu wa miundombinu ya barabara hususani daraja linalounganisha vijiji hivyo na kupelekea kuongeza umbali mrefu kutoka Kijiji kimoja kwenda kingine.
Katika kutatua kero hizo, Mkuu wa wilaya amewataka watumishi wa umma kujenga utamaduni wa kusikiliza na kuwahudumia wananchi ili kutimiza majukumu yao ipasavyo na kuagiza kuundwa kwa dawati la malalamiko ili Watumishi wa umma washuke chini kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao ikiwa ni sehemu ya agizo la Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Watumishi kuwasikiliza Wananchi katika maeneo yao badala ya kukaa ofisini.
Katika Ziara hiyo Mhe Komba amefurahishwa na moyo wa Upendo alio nao Mhe Diwani wa Kata ya Butobela ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kujenga nyumba ya mwalimu shule ya Sekondari Nyakagwe yenye thamani ya Shilingi milioni 38 ambayo aliweza kuweka jiwe la Msingi.
Nyumba ya Mwalimu shule ya Sekondari Nyakagwe iliyojengwa na Kampuni ya Charles Kazungu Plant inayomilikiwa na Mhe Diwani wa Kata ya Butobela Charles Kazungu kwa gharama ya Tsh 38,537,500. Mheshimiwa Kazungu amejenga Nyumba hiyo katika kuunga juhudi za Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuboresha mazingira Mazuri kwa Watumishi wa umma.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa