Na Hendrick Msangi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Cornel Maghembe, amefanya ziara katika kijiji cha Idosero kata ya Lwezera Wilayani huko ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) katika kuwafikia wananchi kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero zinazowakabili.
Katika ziara hiyo Mhe Maghembe aliambatana na watumishi wa Idara mbalimbali za Halmashauri hiyo, kamati ya ulinzi na usalama, diwani wa kata ya Lwezera, mtendaji wa kijiji,mwenyekiti wa kijiji pamoja na viongozi wa chama wa kata hiyo.
Awali akimkaribisha katika Mkutano huo, Diwani wa kata ya Lwezera Mhe Richard Chinchina alimueleza mkuu huyo wa wilaya furaha waliyo nayo yeye kufika kwenye kata hiyo kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea majibu.
“Karibu sana kwenye kijiji chetu cha Idosero kata ya Lwezera, wananchi hawa ni wazawa wa kijiji hiki na wamejitokeza kwa wingi kuja kukusikiliza wakiamini kero zao utazitolea majibu, “alisema Mhe Diwani.
Akizungumza katika mkutano huo ikiwa ni wiki ya kuelekea katika maadhimisho ya siku ya Lishe Kitaifa na uzinduzi wa kampeni ya lishe kwa vijana Balehe octoba 30,2023, Mhe Maghembe aliwataka wananchi hao kuendelea na kilimo cha kisasa ili kuepuka janga la njaa ”Natamani muendelee na kilimo cha kisasa ili Idosero isiwe na njaa.
Serikali imetoa mbolea ya ruzuku na tayari imefika ni nyie kwenda kuchukua kwa bei elekezi, pia mnanipa heshima kuona mnavyojituma mashambani kufanya kilimo, hakutakuwa na mtu wa kuwaletea chakula hivyo nawasihi muendelee kuzitumia mvua zinazonyesha ili kupata chakula cha kutosha na hata kuuza ili kuweza kujenga na kufanya maendeleo.
Mmejifunza kupanda miti ya biashara lakini msije kumaliza maeneo yote kwa kupanda miti hata mkakosa maeneo ya kulima mazao kwa ajili ya chakula”, Alisema Maghembe.
Pamoja na hayo, Mhe Maghembe alisema Serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imekuja na mpango wa kuhakikisha watoto wanapata chakula wakiwa mashuleni na kuwataka wananchi hao kuweka utaratibu mzuri kwa kila kaya kujitoa kuchangia chakula shuleni ili watoto waweze kupata chakula wawapo shuleni.
“Mashamba ya shule yatumike kulima chakula cha watoto, na watakaobainika kushindwa kupeleka chakula kwa ajili ya watoto shuleni watakabiliwa na faini ya kiasi cha shilingi elfu hamsini, au kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja” Alisema Maghembe.
Wananchi wa Kijiji cha Idosero kata ya Lwezera wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya.
Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo na wananchi, Mhe Mkuu wa Wilaya aliwaambia wananchi Serikali yao ipo kwa ajili ya kuwaletea maendeleo na tayari mamilioni ya pesa yameletwa kwa ajili ya kufanikisha miradi mbalimbali zikiwemo fedha za CSR na TASAFKufuatia kero ya kuwa na miundombinu mibovu ya shule ya msingi Idosero, Mhe Maghembe aliiagiza serikali ya kijiji kufanya ukarabati ikishirikiana na wananchi huku yeye akichangia mifuko 10 ya saruji kufanikisha ukarabati huo.
Mkuu wa Wilaya Mhe. Cornel Maghembe akizungumza na wanachi wa Kijiji cha Idosero kata ya Lwezera alipowatembelea kusikiliza kero zao.
Kuhusu kukosa zahanati alimtaka mkandarasi anayejenga Zahanati hiyo ya Idosero kuendelea na ujenzi licha ya changamoto zilizokuwepo ili jengo hilo likamilike na kupunguza kero ya wananchi hao kutembea umbali mrefu kufuata huduma.Ujenzi wa Jengo la Zahanati ya Idosero ambayo ni nguvu za Wananchi. Ujenzi huu ulisimama kwa muda ambapo Mkuu wa Wilaya alimuagiza Mkandarasi kuendelea na Ujenzi.
Aidha kufuatia kero ya kuvunjiwa nyumba kwa walimu wa shule ya msingi Idosero kulikopelekea walimu hao kutokukaa kijijini humo, Mkuu wa Wilaya aliwataka wananchi hao kuimarisha ulinzi shirikishi ikiwa ni pamoja na kuwaonya vijana wao wanaojishughulisha na vitendo vya kiuhalifu ili kuwalinda walimu wanaofanya kazi katika shule hiyo
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa