Geita, Machi 13, 2025 – Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba, amesema ipo haja ya kubadili mfumo wa usimamizi wa miradi inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), hasa miradi inayosimamiwa na Kampuni ya GGML, kutokana na changamoto ya ucheleweshaji wa utekelezaji wake.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika kata ya Nyachiluluma, Komba alieleza kuwa miradi mingi ya CSR haikamiliki kwa wakati, hali inayoweza kuongeza gharama za ukamilishaji wake baadaye.
“Ipo haja ya kubadilisha mfumo wa maamuzi wa CSR. Miradi tunayokabidhiwa inapaswa kulindwa ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, badala ya kuachwa bila usimamizi thabiti,” alisema Komba.
Aidha, Mkuu wa Wilaya aliwataka viongozi wa kata na vijiji kushirikiana kwa karibu na wananchi katika kusukuma mbele maendeleo.
“Sisi tulioajiriwa na serikali hatujaja kuwa juu ya wananchi, bali kuwasikiliza na kuhakikisha hakuna anayebaki na manung’uniko,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Komba amewataka viongozi kuendelea kuimarisha ulinzi shirikishi, ikiwa ni pamoja na vikundi vya sungusungu, ili kulinda amani na utulivu wa jamii. Pia, ametoa siku 14 kwa wasimamizi wa vituo vya maji waliokusanya fedha za wananchi lakini hawajalipa kwa mamlaka husika kuhakikisha wanarejesha fedha hizo ili huduma ya maji iendelee kupatikana bila kikwazo.
Kuhusu masuala ya mikopo, Mkuu wa Wilaya amewasihi wananchi kuepuka mikopo yenye riba kubwa inayojulikana kama kausha damu, akimtaka Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri kuhakikisha fedha za serikali zinazotolewa kwa riba nafuu zinawafikia wananchi waliotimiza vigezo.
Ziara ya Mkuu wa Wilaya inaendelea katika maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Butundwe kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa