Geita, Tanzania
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba, ametoa wito kwa viongozi wa Kijiji cha Busaka na wakazi wake kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata huduma stahiki na msaada kutoka kwa wadau mbalimbali.
Mhe. Komba aliyasema hayo akiwa katika ziara yake ya kawaida katika Kata ya Bukondo, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake katika Tarafa ya Butundwe. “Mnapoona kuna watoto wenye uhitaji maalumu, muwafikie na kuwahudumia ili kwa kushirikiana na wadau, tuweze kuwasaidia,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Abdallah Komba akizungumza na wananchi katika ziara yake Tarafa ya Butundwe Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya alisikiliza na kutatua kero mbalimbali, ikiwemo changamoto ya walimu wanaoishi mbali na shule, jambo linalosababisha uchelewaji wa vipindi darasani. “Hatuwezi kuwa na nyumba za walimu halafu walimu wakae mbali na vituo vya kazi. Lazima tuhakikishe wanakaa karibu ili waweze kuwajibika ipasavyo,” alisema.
Aidha, Mhe. Komba alisifu juhudi za serikali katika kusambaza umeme na kuwataka wananchi waendelee kuiamini serikali katika kukamilisha mpango wa usambazaji umeme kwa vijiji vyote vya Halmashauri.
Miradi Iliyotembelewa
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na:
•Zahanati ya Kijiji cha Chankolongo – Mradi huu umejengwa kwa nguvu za wananchi na fedha za Halmashauri, ukiwa katika hatua ya boma. Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri aliahidi kuwa fedha zitatolewa kwa wakati ili kukamilisha ujenzi huo.
Ziara ya Ukaguzi wa Miradi ikiendelea katika Tarafa ya Butundwe Halmashauri ya Wilaya ya Geita
•Chanzo cha maji cha Chankolongo – Baada ya wananchi kulalamikia upungufu wa maji licha ya chanzo kuwepo kijijini, Mhe. Komba aliiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA) kukagua vituo vyote tisa vya maji na kuhakikisha vinafanya kazi ipasavyo. Pia alimtaka Afisa Tarafa kuandaa mkutano wa uhamasishaji kwa wananchi kuhusu usimamizi wa vituo vya maji.
•Zahanati ya Kijiji cha Kitigiri – Mhe. Komba alisisitiza umuhimu wa kuweka vipaumbele ili kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo kwa haraka.
•Elimu ya Afya juu ya Empox – Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Dkt. Modest, aliwapa wananchi elimu kuhusu ugonjwa wa Empox, akihimiza tahadhari kwa kuepuka kugusana na majimaji ya mwili kama mate na jasho, pamoja na kunawa mikono kwa maji yanayotiririka mara kwa mara.
•Ujenzi wa madarasa – Mkuu wa Wilaya alikagua maendeleo ya vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Lulama, vyumba saba vya madarasa katika Shule ya Msingi Nyasalala, na vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Busaka. Alisisitiza umuhimu wa mamlaka husika kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati.
Mhe. Komba aliendelea kuwasihi viongozi na wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akiahidi kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa