Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Paul Wanga amelishauri baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Geita kufikiria kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo kwa kujenga vyuo vya Veta vitakavyokuwa vinafundisha stadi za uchimbaji wa madini ili kuwasaidia vijana kuwa na ujuzi wa shughuli hizo.
John Wanga ameshauri hayo leo Agosti 12, 2021 wakati akihutubia baraza la madiwani kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake kuwa mkurugenzi wa wilaya ya Geita,ambapo ameweka wazi vipaumbele 14, ambavyo atajielekeza yeye kama mkurugenzi na watendaji wake kuvitekeleza.
Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa madiwani kuwa Zaidi ya kata 10 katika wilaya ya Geita zinajihusisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu, amesema kuwa kuwapa elimu na ujuzi sahihi wa shughuli hizo, kutaisaidia Halmashauri ya wilaya ya Geita, kuwa na mapato ya kutosha kutokana na uchimbaji wenye tija,huku akiwataka madiwani kuwa na mawazo kama hayo ili kuwasaidia wananchi.
Amesema kuwa atahakikisha Halmashauri inawawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo amabayo ni asilimia 10 ya mapato ya ndani, kwa makundi maalumu kama vijana, wanawake na watu wenye ulemavu,ambapo fedha zote zitakazotolewa zinatakiwa kuzunguka kwa wahusika na kurejeshwa,huku akieleza kuwa ni vyema ikagawiwa fedha nyingi kwenye kikundi cha watu ili fedha hizo za mikopo zilete matokeo kwa wananchi kitu ambacho hata viongozi wengine wa juu wanatamani kukiona.
Aidha mambo mengine ya kujielekeza katika utumishi wake aliyoyaeleza,ni pamoja na utawala,kukusanya mapato ya ndani,kukuza kilimo,uvuvi,mifugo,upimaji wa ardhi ili kuwa na makazi bora,kuboresha elimu na afya.
Mengine ni pamoja na kuimarisha usafi wa mazingira kuanzia ngazi za chini,kuboresha na kujenga miradi ya maji ili wananchi wapate maji safi na salama ,ujenzi wa majengo na barabara,miradi mikubwa ya vielelezo,na nishati ya umeme huku akisisitiza kuwa ‘wakandarasi wazembe hawana nafasi katika wilaya hii’
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa