Na: Hendrick Msangi
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Karia Rajabu Magaro ametoa maagizo mazito kwa kamati za ujenzi, wazabuni na mafundi wanaotekeleza miradi mbalimbali katika Halmashauri hiyo.
Magaro ametoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akikagua maendeleo ya miradi ya shule kwenye kata mbalimbali za Halmashauri hiyo zinazojengwa kwa fedha za SEQUIP.
Ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake kufanya ziara kwenye miradi hiyo, Magaro alibaini uzembe unaotokana na kutokuwa na uwazi katika utekelezaji wa miradi hiyo unaosababishwa na mafundi waliopewa kazi za ujenzi, kamati zinazosimamia miradi hiyo ambazo zimekuwa zikichelewesha kupeleka vifaa na kupelekea mafundi kukaa bila kufanya kazi, pamoja na wazabuni ambao wamepewa jukumu la kusambaza vifaa vya ujenzi kwenye miradi hiyo.
Mradi wa Shule ya Sekondari Nyakaduha kata ya Nyakaduha Wilayani Geita. Shule itaanza kupokea wanafunzi 120 kidato cha kwanza ifikapo Januari 2024
Alisema kamwe hawezi kukubaliana na uzembe wowote ambao unakwamisha kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ya shule ya Sekondari Nyakaduha na shule ya Sekondari iliyopo kata ya Ludete ambapo amesema serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi hiyo ili watoto wa kitanzania wapate elimu katika mazingira mazuri.
“Uzembe wowote unaosababishwa katika miradi hii sitaufimbia macho, watachukuliwa hatua wote wanaokwamisha kasi ya ukamilishwaji wa miradi, hatuwezi kwenda kwa kubembelezana tunafanya kwa faida ya watoto wetu, fedha zipo toka mwezi wa sita, natoa maagizo kwa kamati za ujenzi ifikapo Novemba 30 mkabidhi kazi kwani muda uliowekwa kukamilisha ujenzi umekwisha” alisema Magaro.
Aidha aliziagiza kamati za ujenzi, kutokuwalipa mafundi wote wanaosababisha hasara kwenye miradi hiyo na badala yake fedha hizo zitumike kufanya kazi nyingine za miradi hiyo.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo alikagua vifaa vya ujenzi yakiwemo matofali kuona ubora wake ili kuepuka athari ambazo zinaweza kujitokeza kwenye majengo na kuwaagiza wahandisi kutokupokea vifaa kutoka kwa wazabuni ambavyo vipo chini ya kiwango mpaka watakapothibitisha ubora wake kabla ya malipo kufanyika.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Karia Rajabu Magaro( aliyesimama) akikagua ubora wa matofali katika shule ya Sekondari iliyopo kata ya Ludete. Mradi wa Shule una thamani ya shilingi 584,280,029
Akiendelea kukagua miradi hiyo alizitaka kamati hizo kufanya kazi kwa kushirikiana na kwa uwazi ikiwa ni pamoja na kuwasimamia mafundi na sio kuwaacha kujipangia muda wa kufanya kazi jambo ambalo linachelewesha ukamilishwaji wa majengo ya shule hizo.
Mkurugenzi huyo aliwatembelea wazabuni wote waliopewa kazi za usambazaji wa vifaa kwenye miradi ya shule hizo ili kuona utekelezaji wao ikiwa ni pamoja na kujua changamoto ambazo zinazowafanya kutokupeleka vifaa kwa wakati katika miradi waliyopewa.
Ukaguzi Mradi wa Shule ya Sekondari kata ya Ludete Wilayani Geita.
Kwa upande wa mradi wa jengo la utawala ambalo ofisi za Halmashauri zimejengwa , Magaro aliagiza watu wa manunuzi na wahandisi kuhakikisha kazi zote zilizobaki zinakamilishwa kwa haraka na mafundi wawepo eneo la kazi (site) ili mpango wa kuhamia katika jengo hilo ukamilike kwa uharaka.
Halmashauri ya wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru serikali inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwenye halmashauri hiyo kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo ili waendelee kuwa na Imani na serikali yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa