Nzera-Geita
MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Rajab Magaro ametoa rai kwa wananchi Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuchangamkia fursa ya Mikopo isiyokuwa na riba inayotolewa na Serikali ya awamu ya Sita kupitia Halmashauri.
Magaro ameyasema hayo katika uzinduzi wa utoaji wa mikopo na vitambulisho vya wajasiliamali ulio fanyika katika viwanja vya Halmashauri-Nzera Februari 10, 2025.
“Ni faraja kubwa kwa Halmashauri kutekeleza hatua hii muhimu ya Serikali ya kutoa mikopo ya asilimia 10. Muongozo wa Serikali unasema kila bajeti ya mwaka tutenge fedha za miradi ya Maendeleo na fedha za Mikopo ya vikundi vya wanawake vijana na watu wenye ulemavu " Amesema Magaro.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Rajab Magaro akizungumza na wananchi waliojitokeza katika hafla ya utoaji mikopo.
Aidha Ndg Magaro amesema Halmashauri imetenga Kiasi cha Shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya wananchi ambao watakidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.
“Leo tuna toa Mikopo ya kiasi cha Shilingi Milioni 689,000,000 ikawe hamasa kwa wana kikundi wengine kujitokeza kuja kukopa" Amesema Ndg Magaro.
Wananchi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakiwa katika viwanja vya halmashauri wakati wa hafla ya ugawaji mikopo.
Pamoja na hayo Magaro ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utaratibu mpya aliouweka wenye uwazi kusimamia mikopo hiyo.
“Niwaombe wote mlionufaika na mikopo muweze kuandika kila mnachokifanya katika biashara zenu ili Wataalam watakapopita kuwatembelea waweze kuwapa ushauri"
Vilevile Magaro ame wasihi wana vikundi hao kuhakikisha wanatoa taarifa Pale wanapopata changamoto kwa kuwashirikisha Wataalam kutoka Halmashauri ili waweze kuwakwamua kwani Halmashauri ipo tayari wakati wote.
"Tuna amini kuwa mtakuwa chachu kwa kuhakikisha makubaliano yale mnayoyafanya mnayatekeleza kwenye miradi yenu mliyofungua na kusimamia marejesho kufanyika kwa wakati ili wananchi wengine waweze kunufaika na mikopo hii" Ameongeza Magaro.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu ameishukuru serikali kwa kurejesha mikopo hiyo toka Septemba 2024.
“Sisi Madiwani kazi yetu kubwa ni kusimamia na kuhakikisha fedha inatengwa kwa taratibu zilizowekwa kwa kila bajeti. Halmashauri itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya makundi ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu” Amesema Mhe Kazungu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu akizungumza na wananchi katika hafla ya utoaji mikopo
Vilevile Mhe Kazungu amevitaka vikundi hivyo kuitumia mikopo hiyo katika malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kurejesha kwa uaminifu na kupelekea kupunguza idadi ya vijana walio mtaani kwa kujikwamua kiuchumi.
“Ni wasihi mkawe waaminifu kurejesha mikopo ili kuendelea kutoa fursa kwa wana Geita wengine kupata mikopo hiyo na mkawe kielelezo kizuri kwa wengine” Amesema Mwenyekiti
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Geita Komredi Michael Msuya ametoa wito kwa Halmashauri na Taasisi za umma kuwapa fursa wana vikundi hao pale ambapo kuna kazi wanazoweza kuzifanya zikiwepo usambazaji wa chakula katika shule zinazohitaji chakula, shughuli za useremala na nyinginezo ili waweze kurejesha mikopo hiyo kwa wakati
Msuya amesema ili tija ya Mama Samia Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa itimie ni wajibu kwa maafisa maendeleo kuwasimamia wana vikundi hao ili waweze kutimiza malengo ya vikundi vyao.
Hali kadhalika Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Jonas Kilave amesema katika hafla hiyo kuwa jumla ya vikundi 39 vimekidhi kupata Mikopo ambapo vikundi vya wanawake 23 vimepatiwa kiasi cha shilingi Milioni 351, vikundi vya vijana 14 kiasi cha shilingi milioni 293 na vikundi vya watu wenye ulemavu 2 vikipewa kiasi cha shilingi milioni 45 na kufanya jumla ya kiasi cha shilingi milioni 689 kutolewa.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Jonas Kilave akiwasilisha taarifa ya utoaji wa mikopo kwa Halmashauri
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa