Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg Karia Magaro Novemba 18, 2024 ameongoza timu ya menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya Geita kukagua miradi ya maendeleo katika kata za Nyamigota, Ludete na Katoro zilipo jimbo la Busanda.
Timu hiyo imetembelea na kukagua ujenzi wa shule ya amali iliyopo kata ya Nyamigota kijiji cha Chibingo mradi wenye thamani ya Shilingi Milioni 584,280,029 ili kuona hali halisi ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Amali ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Nyamigota Mwl Renatus Martini (wa pili kulia) akitoa maelekezo ya maendeleo ya mradi Mbele ya Timu ya menejimenti ya Halmashauri iliyoongozwa na Mkurugenzi mtendaji Ndg. Karia Magaro
Aidha timu ya menejimenti imetembelea mradi wa upanuzi wa miundombinu ya kidato cha 5 na 6 shule ya sekondari Kagega wenye thamani ya shilingi Milioni 481, upanuzi wa miundombinu ya kidato cha 5 na 6 shule ya sekondari Lutozo mradi wenye thamani ya shilingi Milioni 381 na mradi wa shule ya msingi mtaa wa afya ambayo ilianza kwa nguvu za wananchi na baadaye kuendelezwa madarasa 9 kwa mfuko wa BOOST kwa thamani ya Milioni 351.5.
Timu ya menejementi ya Halmashauri ikikagua mradi wa ujenzi wa nyumba za waalimu katika shule ya Kagega iliyopo kata ya Ludete
Mwonekano wa madarasa katika mradi wa Upanuzi wa kidato cha tano na cha sita katika shule ya sekondari Lutozo
Pamoja na miradi hiyo, timu iliweza kutembelea Kata ya Katoro eneo ambalo litajengwa shule ya sekondari ya kata ambapo kwa sasa ipo hatua za awali. Mradi huo una jumla ya kiasi cha shilingi Milioni 584,280,029.
Katika ukaguzi wa miradi hiyo timu ilibaini kuwepo kwa changamoto zinazosababishwa na wazabuni kwa kuchelewesha vifaa vya ujenzi kwenye miradi na hii ni kutokana na wazabuni hao kushinda tenda katika maeneo mengi ilihali hawana uwezo wa kusambaza vifaa kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita akikagua ubora wa tofali katika mradi unaendelea kujengwa shule ya sekondari Lutozo.
Kufuatia changamoto hiyo, timu ya menejimenti iliwafuatilia wazabuni hao na kuwapa muda maalum wa kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinafika kwenye miradi ili mafundi ujenzi waweze kuendelea na kazi na miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuanza kutumika kama ambavyo mikataba ya ujenzi inavyowataka.
“Hizi kazi ni za Halmashauri hivyo niwatake mnapotangaza tenda kwenye mfumo wa Nest muangalie uwezo wa wazabuni katika kukamilisha kazi wanazoziomba katika Halmashauri ili kuepusha kuchelewesha miradi” amesema Magaro
Fundi Deogratius Wilson ni mmoja wa mafundi wanatekeleza miradi iliyotembelewa na timu ya menejimenti ambapo amesema wanatumia muda mwingi kuwepo uwandani (site) bila ya kuwepo kwa madini ujenzi kutokana na wazabuni kutokupeleka vifaa kwa wakati jambo ambalo lina wagharimu katika kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Kwa upande wake Scolastika Vitalis ambaye ni mmoja wa wanakamati wanaosimamia miradi ameileza timu ya menejimenti adha wanayoipata kutokana na wazabuni kutokusambaza madini ujenzi kwa wakati na kuwafanya kukaa uwandani(site) bila kazi yoyote.
Kufuatia changamoto hizo Ndg Magaro ametoa maagizo mazito kwa wazabuni hao ikiwa ni pamoja na kufika kwenye ofisi zao akiwa na timu ya menejimenti na kuwataka kusambaza vifaa kama ambavyo mikataba yao ipo na iwapo watashindwa basi mikataba yao itaenguliwa na kazi hizo kupewa wazabuni wengine.
Pamoja na hayo Mkurugenzi amewataka walimu ambao wana simamia miradi hiyo kuhakikisha ubora wa vifaa vinavyoletwa na wazabuni hao vina ubora unaostahili ikiwa ni pamoja kusimamia kila hatua ya ujenzi kwa kushirikiana na kutoa taarifa mahali penye changamoto ili miradi isisimame na wanafunzi waweze kuitumia ifikapo mwakani.
Huu ni utaratibu unaofanywa na Mkurugenzi Mtendaji kwa kushirikiana na timu ya menejimenti kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuendelea kuweka msukumo katika ukamilishwaji wake
Halmashauri ya wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa