Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita Januari 14, 2022 imefanya ziara ya kukagua Miradi iliyojengwa kwa fedha za UVIKO 19 katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kueleza kuridhishwa na ubora wa Miradi hiyo.
Kiongozi wa msafara wa ziara hiyo ambaye ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa kutoka Mkoa wa Geita Bw.Evarist Gervas ameeleza wazi kuridhishwa na thamani na ubora wa Miradi hiyo huku akiisifu Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Miradi hiyo.
Bw.Evarist amesema kuwa Viongozi wana wajibu wa kutangaza mazuri yaliyofanywa na Serikali ili jamii itambue namna Rais Samia anavyowajali wananchi wake kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ya jamii kama alivyofanya kupitia Fedha za UVIKO 19.
Aidha ametoa wito kwa Wazazi kuhakikisha wanadhibiti utoro kwa kuwapeleka watoto wao shuleni sambamba na kuwataka walimu kufundisha kwa bidii ili madarasa hayo yaliyojengwa kwa gharama kubwa na ubora wa hali ya juu yalete matokeo mazuri.
Bw.Evarist akiwa katika kata ya Rwamgasa alipotembelea Mradi wa vyumba 14 vya madarasa katika shule ya sekondari Isingiro ameunga mkono juhudi za wananchi katika kuchangia Maendeleo kwa kutoa kiasi cha shilingi laki tano ambapo awali alitoa wito wa kusimamia vizuri Miradi ya maendeleo inayojengwa kwa nguvu za wananchi ili iwe na ubora kama Miradi inayoletewa fedha na Serikali Kuu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe.Wilson Shimo akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita ameendelea kutoa shukrani kwa Rais Samia kwa fedha nyingi alizoupatia Mkoa wa Geita huku akiwataka wananchi kutembea vifua mbele kwa kuwa hakuna vikwazo kwa watoto wetu kuanza kidato cha kwanza.
‘‘Shime wazazi tuwapeleke na kuwahimiza watoto wetu kuja shuleni kusoma shule zitakapofunguliwa na mwisho tutegemee ufaulu kwani kwa miundo mbinu hii mizuri, ni wazi mwanafunzi atakayeanzia kusomea humu sidhani kama atafeli ”.
Naye mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi Mkoa wa Geita Bw.Lucas Mazinzi amechangia mifuko 10 ya Saruji katika shule hiyo ya sekondari Isingiro huku akiisifu Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kazi kubwa ya usimamizi wa ujenzi wa Miradi hiyo iliyofanywa usiku na mchana huku akiomba kupewa mbinu ya ufanisi kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilikuwa na Miradi mingi zaidi ingawa imekamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Paul Wanga akiwa katika ziara hiyo amemshukuru Rais Samia kwa kuipatia Halmashauri hiyo kiasi cha shilingi Bilioni 7 na Milioni 120 kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2021 iliyowezesha kujenga Miradi mbalimbali ya maendeleo.
Fedha hizo zimesadia kukamilisha ujenzi wa vyumba 347 vya madarasa kwa shule 44 za sekondari na vyumba 5 vya madarasa kwa ajili ya shule mbili shikizi za msingi na bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule ya sekondari Katoro.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe.Charles Kazungu akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara hiyo ameshukuru kwa pongezi zilizotolewa kwa Halmashauri hiyo huku akiahidi kutobweteka na badala yake wataendelea kutekeleza kikamilifu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi sambamba na kupokea ushauri wanaopewa na viongozi mbalimbali.
Kamati hiyo ya Siasa Mkoa wa Geita ilitembelea na kukagua Miradi ya ujenzi wa kituo cha Afya Bugalama wenye thamani ya shilingi milioni 250, Mradi wa vyumba 13 vya madarasa katika shule ya sekondari Bugalama wenye thamani ya shilingi milioni 260, na Mradi wa vyumba 8 vya madarasa katika shule ya sekondari Chigunga wenye thamani ya shilingi milioni 160.
Aidha kamati hiyo iliendelea kukagua Mradi wa vyumba 6 vya madarasa katika shule ya sekondari Butundwe wenye thamani ya shilingi milioni 120, na kuhitimisha na Mradi wa vyumba 14 vya madarasa katika shule ya sekondari Isingiro wenye thamani ya shilingi milioni 280 amabapo kamati hiyo imeridhishwa na miradi yote hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa