Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba ametoa wito kwa Halmashauri kuhakikisha ajenda ya ushiriki wa wananchi kwenye Uchaguzi inapewa kipaumbele ili waweze kujitokeza kupiga kura.
Akizungumza tarehe 28, Julai 2025 kwenye ukumbi wa EPZ-Bombambili ambapo aliendesha kikao maalumu cha kufanya majumuisho ya maandalizi ya mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, 2025 na Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na wa Manispaa ya Geita, taasisi zenye miradi, sambamba na wadau na kamati za Mwenge, Mhe. Komba ameziagiza Halmashauri hizo kuja na ubunifu wa kuhakikisha ujumbe wa Uchaguzi unakuwepo na elimu inatolewa ya kutosha kwenye kila mradi ambao utatembelewa na Mwenge huo.
Mhe. Komba pia ameagiza vikao vya maandalizi ngazi ya Kata na Vijiji vianze mapema kupitia kwa Watendaji ili kuwahamasisha wananchi na makundi yote muhimu kujitokeza kwenye maeneo ambayo yatapitiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg. Karia Magaro amewataka watumishi kufanya kazi kwa kushirikiana, pamoja na kujitokeze kwa wingi kuulaki Mwenge.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (W), CDE Michael Msuya amesema kuwa chama kitashirki kwa kutoa msukumo haswa kwenye eneo la hamasa kwa vijana, huku akitoa msisitizo kwa Wakuu wenye miradi kuhakikisha nyaraka zinakaa vizuri.
Takribani Kilomita 82.7 zinatarajiwa kupitiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, huku ukitembelea miradi mbali mbali kwenye sekta za Afya, Elimu, Maji, Utawala pamoja na Barabara.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa