Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mh. Hashim Abdallah Komba, amewasisitiza watumishi wa umma kuwa mstari wa mbele kwenye kusikiliza kero za wananchi, na kutafuta namna bora ya kutatua changamoto zao ambazo wamekua wakikumbana nazo mara kwa mara kwenye maeneo yao.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mh. Hashim Komba akizungumza na wananchi wa Kata ya Chigunga, Tarafa ya Butundwe.
Akizungumza mwishoni mwa juma liliopita katika Kata ya Chigunga wakati akihitimisha Ziara ya Kikazi iliyohusisha Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo sambamba na kutatua kero za wananchi wa Tarafa ya Butundwe Wilayani Geita, Mh. Komba amewataka Watumishi, hususan Watendaji wa Kata na Vijiji, kutotumia mabavu, na badala yake kuwa wanyenyekevu pindi wanapotoa huduma kwa wananchi.
"Ni wajibu wa Kila mtumishi wa umma, kushuka chini, kujinyenyekeza na kuwasikiliza wananchi. Serikali ya awamu ya sita, haitaki utawala wa mabavu na kutozingatia Sheria. Niwasihi watumishi wenzangu tuwasikilize wananchi kwasababu serikali imepata uhalali wake kwa wananchi kwenda kuipigia kura." Amesema Mh. Komba.
Aidha, Mh. Komba pia amewataka Watendaji kuhakikisha wanazingatia suala la uadilifu kwenye matumizi ya fedha za maendeleo huku akiwasihi viongozi kusimamia vyema rasilimali za serikali.
Kwa upande mwingine, Mh. Komba pia ameagiza Idara ya Maendeleo ya Jamii kuhakikisha inatafuta namna bora ya kuwaanzishia miradi watu wenye mahitaji maalum ili iwe rahisi kwao kusimamia na kujiingizia kipato kitakachowainua kiuchumi ambapo serikali pia imerahisisha masharti na vigezo vya vikundi hivyo kupata mikopo.
Habari Picha ya Matukio yaliyojitokeza wakati wa Ufungaji wa Ziara ya Kikazi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mh. Hashim Komba, Tarafa ya Chigunga.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa