Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Geita Mh. Charles Kazungu amehimiza suala la ushirikiano baina ya watendaji wa halmashauri katika ukusanyaji wa mapato ili kuleta ufanisi pamoja na kuziwezesha halmashauri kujiendesha kutokana na shughuli za kiuchumi zinazopatikana ndani ya halmashauri hizo.
Akizungumza hii leo katika kikao cha mafunzo ya ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini ya dhahabu kilichoandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kuhudhuriwa na Wabunge, Wenyeviti, Wakurugenzi, Madiwani, na Watumishi kutoka Halmashauri za Wilaya ya Nsimbo na Kilwa, Mh. Charles Kazungu amesema kuwa ipo haja ya halmashauri kushirikiana, pamoja na kubadilishana ujuzi wa namna bora ya ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini ili kuleta ufanisi katika sekta hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mh. Charles Kazungu amesema kuwa, suala la mpango wa wajibu wa Kampuni kubwa za migodin kurejesha kwa jamii (CSR), linatokana na kanuni, na kwamba masoko yote ya Dhahabu Wilayani Geita yanaratibiwa chini ya Tume ya Madini.
"Ipo haja ya sisi kama Halmashauri kushirikiana, pamoja na kubadilishana uzoefu wa mara kwa mara ya namna gani tunaweza kuongeza mapato yetu ya ndani, haswa kwenye sekta ya madini. Kazi ya kukusanya mapato sio rahisi na hivyo tunapaswa kutoa elimu pia kwa wachimbaji pamoja na kuweka mazingira rafiki ya wao kufanya kazi." Amesema Mh. Kazungu.
Mh. Kazungu pia amesema kuwa sheria bado inafanyiwa kazi ili kusudi wachimbaji wadogo waweze kupata leseni ndogo za uchimbaji (PL) huku wao kama Halmashauri wakiwa na jukumu la kutoa wataalamu wakufanya tathmini ya ardhi kwaajil ya shughuli za uchimbaji.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Geita, Ndg. Karia Magaro: Timu ya Menejimenti ya Halmashauri (CMT) iliona umuhimu wa kuwa na kikosi kazi (Task Force), ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na hivyo kurahisisha kazi ya ukusanyaji wa mapato.
Aidha, Diwani wa Kata ya Bugulula, Mh. Lupuga Haraka, amesema kuwa ipo haja ya kutungwa kwa sheria ndogo ili kufanikisha zoezi la ukusanyaji wa mapato, ushirikishwaji wa wananchi haswa vijana kwa maeneo ambayo yanazungukwa na migodi, pamoja na uundwaji wa Kamati za Madini kwenye Halmashauri zenye shughul za uchimbaji wa madini.
Afisa Misitu na Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya, Geita Bi. Hellen Eustace amefafanua ya kuwa, Mfanyabiashara anayefanya shughuli za kuuza Magome ya miti (Timber) yanayotumika kama ngazi wakati wa uchimbaji, anapaswa awe amesajiliwa na Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS) ili kutambua mahali anapofanyia biashara pamoja na leseni ya mahali anapovuna timba.
Kwa upande wake, Afisa Masoko kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Bw. Mohamed Wangeleja amesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na tija kwa kuwa yamewapa mbinu tofaut za ukusanyaji wa mapato, ambazo zitaenda kutumika katika Halmashauri zao na hivyo kuongeza ufanisi kwenye zoezi la ukusanyaji wa mapato.
"Mafunzo yanaelemisha na kile tulichotaraia kuja kujifunza tumekipata. Hivyo tutaenda kukifanyia kazi na kuhakikisha kile ambacho wenzetu wamefanikiwa kukifanya, na sisi tunaenda kukiwekea utaratibu ili kuweza kuongeza mapato kwenye Halmashauri zetu, haswa kwenye sekta ya madini." Amesema Bw. Mohamed.
Maafisa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa wakichangia mada kwenye kikao cha mafunzo ya ukusanyaji wa mapato Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Ukusanyaji wa mapato kwenye shughuli za uchimbaji wa madini hutofautiana kila mwaka kutokana na mlipuko wa dhahabu unavyotokea, na hivyo ukaguzi wa maeneo yanayodhaniwa kuwa na dhahabu hufanyika mara kwa mara ili kubaini maeneo mapya yanayoibuka na kudhibiti utoroshwaji wa mapato.
Bi. Eveline Mtahamba (Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya, Geita): Tumeanzisha masoko mengi ya ukusanyaji wa ushuru wa huduma (Service Levy) kwa wachimbaji wadogo kutokana na uhitaji kuwa mkubwa, ambapo masoko hayo yapo katika kata za Katoro, Rwamgasa, Nyarugusu, Nyakagwe na Nyaruyeye.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa