Na Hendrick Msangi
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (MB), Desemba 16, 2023 amefanya ziara ya kikazi Mkoani Geita ambapo katika ziara hiyo amefanya kikao na viongozi wa Mkoa pamoja na kuzungumza na Watumishi wa sekretarieti ya Mkoa.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo wakifuatilia hotuba ya Waziri Mchengerwa.
Katika kikao hicho ambacho Halmashauri zote za Mkoa wa Geita zilishiriki zikiongozwa na wenye viti wa Halmashauri,Wakurugenzi watendaji, pamoja Wakuu wa Wilaya, ziliweza kukabidhiwa magari matano ya usimamizi wa shughuli za Afya pamoja na vifaa vya TEHAMA kwa vituo vya walimu kwenye Halmashauri zote za mkoa wa Geita.
Mhe Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mohamed Omary Mchengerwa (MB) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Cornel Magembe funguo za gari kwa ajili ya usimamizi Shirikishi kwa Shughuli za Afya.
Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kuwataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii katika maeneo yao, ili kumtendea haki Mhe Rais kwa kuwasikiliza wananchi kero zao, kuwa na nidhamu kazini, kujishusha, kuwa wanyenyekevu , kuwa na huruma, kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo hupelekea mambo mengi kuharibika na kusababisha serikali kuchukiwa. “Atakaye fanya kazi kwa bidii tutamlinda kwa nguvu zetu zote kwa kumsaidia kwa kuwa anafanya kazi vizuri na kwa bidii” alisema Mhe Mchengerwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Geita ndg Karia Rajabu Magaro akipokea Kompyuta kutoka kwa Waziri wa nchi OR-TAMISEMI Mhe Mohamed Omary Mchengerwa kwa ajili ya Vituo vya Walimu kwenye Halmashauri za Mkoa wa Geita.
Akiendelea katika hotuba yake kwa watumishi hao, Mhe Mchengerwa (MB), aliwaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa huo kuwa na mpango wa kuandaa vyanzo vipya viwili vya mapato ambavyo kila Mkurugenzi atapimwa kwa namna ambavyo ataweza kubuni vyanzo vipya vya mapato.”Wakurugenzi muende mkajipange kila mwaka tutakuwa tuna angalia umekuja na vyanzo vipya vya mapato na iwapo vitakuwa havijatimia itapelekea kuwekwa pembeni ama kutafutiwa kazi nyingine itakayakutosheleza kutokana na uwezo wako”, alisema Mhe Waziri.
Kuhusu swala la Miradi ambayo serikali inatenga fedha nyingi, Mhe Mchengerwa alisema zitaandaliwa fomu maalumu ambazo Mkurugenzi, Mhandisi na mtu wa Manunuzi watazisaini kama uthibitisho wa kukubali fedha hizo kutosheleza kutekeleza miradi iliyopangwa ili kuepuka upotevu wa fedha ambao umekuwa ukijitokeza maeneo mengine na kusababisha kutokamilika kwa miradi.
Aidha aliwataka Wakurugenzi Katika mpango wa maendeleo kutenga bajeti kwa ajili ya watumishi wanaoenda likizo kwa kuwaandalia stahiki zao na sio kuwakopesha kuepusha makasiriko kwa watumishi na kuepelekea watumishi kuichukia serikali yao.
Pia alielekeza fedha zinazokusanywa kutenga asilimia zitakozokwenda kwenye mipango ya maendeleo katika Halmashauri zao na sio kusubiri bajeti ya serikali.
Pamoja na kukabidhi magari hayo, Mhe Mchengerwa (MB), ametoa wiki mbili kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambao hawaishi kwenye maeneo yao ya kazi kunakopelekea wananchi kukosa huduma kwa wakati kurejea kwenye maeneo yao na iwapo watashindwa kufanya hivyo watahamishwa kupelekwa maeneo mengine, huku akimuagiza Mkuu wa Mkoa Ndugu Martine Shigela kuandaa taarifa ya watumishi ambao hawakai maeneo yao ya kazi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini Mhe Joseph Musukuma ambaye aliwawakilisha wabunge wa mkoa huo, aliipongeza serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo alisema amefarijika sana kushirki kikao hicho ambacho Mhe Waziri alikabidhi magari kwa Halmashauri za Mkoa huo nakuishukuru Serikali kwa niaba ya watumishi wa Mkoa huo, “ Hakuna Jimbo linalomdai Mhe Rais kwani tuna miradi mingi, Mhe Rais ametoa pesa kujenga Uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Mwanza pamoja na daraja ambapo kukamilika kwake kutawezesha watalii kufika kwenye vivutio vya utalii vilivyopo Mkoani Geita kwa urahisi,” alisema Musukuma
Mkuu wa Mkoa Ndugu Martine Shigela aliishukuru serikali inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuchangia huduma za elimu bila malipo katika Mkoa wa Geita, ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo SEQUIP, BOOST, UVIKO na nyingine kutoka serikali kuu amabapo Mkoa wa Geita umepokea fedha nyingi zaidi ya Bilioni 47 ambazo zimewezesha kujenga shule mpya Zaidi ya 18 kwani ndio msingi wa maendeleo kwenye Taifa letu, Kwa upande wa Afya, Shigela alisema Mkoa wa Geita una Baraka kwani kuna Hospitali mbili za Wilaya moja ikiwa Nzera na nyingine Katoro zote zikiwa kwenye jimbo la Mhe Musukuma(MB) huku akitaja hospitali nyingine katika Halmashauri za Mbogwe, Nyang’wale, Bukombe ambapo zote serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.
Mkuu wa Mkoa wa Geita ndg Martine Shigela akiongea na Watumishi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Geita wakati wa Ziara ya Kikazi ya Mhe Waziri wa nchi OR-TAMISEMI alipotembelea Mkoa wa Geita.
Kuhusu swala la Lishe Mhe Mkuu wa mkoa alimueleza Mhe Waziri kuwa Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa mitano ambayo haikufanya vizuri kwenye swala la lishe , ambapo hatua madhubuti zimeshachukuliwa kwa kuweka mikakati pamoja na kuwa na nyenzo zote zinazohitajika kwenye vituo vya afya ikiwa ni pamoja na kuongeza hamasa.
Aidha alimuahidi Mhe Waziri kuyatunza Magari ambayo Serikali imetoa kwa Mkoa wa Geita zikiwepo Ambulance mbili ambazo tayari zimeshaanza kutoa huduma kwenye Halmashauri ya Mbogwe na Nyang’wale na mengine ambayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (MB) aliyakabidhi.
Naye msimamizi Mkuu wa shughuli za afya, Lishe na Ustawii katika Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Dkt Modest Buchard, alitoa shukrani kwa awamu ya sita kwa kutoa magari matano ya usimamizi shirikishi kwa shughuli za afya na kumuahidi Mhe waziri kwenda kufanya kazi, kutumika ili kuendelea kumuunga mkono Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwani sio jambo ambalo limezoeleka.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa