Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) , katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria , imefanya kikao na wadau wa uchaguzi kutoka Halmshauri ya Wilaya ya Geita , kwa lengo la kujidhirisha kuhusu mchakato wa kugawa jimbo la Busanda kama ulifuata taratibu na vikao vya sheria.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita , Jaji wa Mahakama Kuu Mhe Asina Omari , kwa niaba ya mwenyekiti wa INEC , alisema kuwa tume ilipokea tume ilipokea rasmi maombi ya kugawa jimbo la Busanda kutoka kwa katibu tawala wa mkoa wa geita mnamo tarehe 28 februari 2025.
Jaji wa Mahakama Kuu Mhe Asina Omari na mjumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi akizungumza katika Kikao cha Mchakato wa Kugawa Jimbo la Busanda kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita
Kwa mujibu wa kanuni ya 18 ya kanuni za Tume ya mwaka 2024 , Jaji Asina alibainisha kuwa tume imeamua kutembelea baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa ili kuhakikisha kuwa taarifa zilizowasilishwa ni sahihi na zinazingatia taratibu husika.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia Ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim Komba (Kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ndg Karia Magaro wakati wa kikao cha Mchakato wa Ugawaji wa Jimbo la Busanda kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita
Katika kikao hicho , Adam Mkina , mwakilishi wa Mkurugenzi wa INEC , alitoa ufafanuzi kuhusu majina ya majimbo ,kata zinazohusika pamoja na ramani ya eneo linalopendekezwa kugawanywa. Wajumbe wa kikao hicho walithibitisha kuwa taarifa zilizowasilishwa na uongozi wa INEC zinaendana na maamuzi ya vikao vilivyopita na ni sahihi.
Bw. Adam Mkina , Mwakilishi wa Mkurugenzi wa INEC , alitoa ufafanuzi kuhusu majina ya majimbo katika Kikao kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Mchakato huu wa kugawanywa kwa jimbo la Busanda umelenga kuboresha uwakilishi wa wananchi bungeni pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kijamii. Jimbo la Busanda, ambalo limekuwa na ukubwa wa eneo na idadi kubwa ya wakazi, limekuwa likipokea maombi kutoka kwa viongozi na wananchi kuhusu kuligawa ili kuongeza uwakilishi na kuharakisha maendeleo.
Aidha , Wajumbe pia walitoa wito kwa serikali na mamlaka husika kuchukua jukumu la kuhakikisha kuwa mchakato huu unasimamiwa kikamilifu kwa uwazi na kwa kufuata taratibu zote, hadi pale majibu ya mwisho yatakapotolewa kuhusu hatma ya kuligawa Jimbo la Busanda. Wamesisitiza kuwa ni muhimu kila hatua ya mchakato huu ifanyike kwa kuzingatia usawa, maoni ya wananchi, na madhara chanya kwa maendeleo ya maeneo yote yanayohusika. Aidha, waliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoa mrejesho kwa umma mara baada ya uchambuzi wa maoni kukamilika, ili wananchi wafahamu uamuzi wa mwisho na sababu zilizozingatiwa.
Pichani ni Wajumbe mbalimbali wakifuatalia Mchakato wa Ugawaji wa Jimbo la Busanda
Jaji Asina Omari, akitoa neno la mwisho katika mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa kufuata misingi ya haki, usawa na ushirikishwaji katika mchakato mzima wa kuligawa Jimbo la Busanda. Alieleza kuwa, "Mchakato huu si wa kisiasa bali ni wa kimaendeleo, na ni lazima usimamiwe kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi ananufaika na uamuzi utakaofanyika. Tume yetu itazingatia kila hoja, kila maoni, na kila ushahidi uliowasilishwa kabla ya kutoa mapendekezo ya mwisho."
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa