Baada ya hivi karibuni Waziri mkuu Kassim Majaliwa kufungua soko kubwa la dhahabu mkoani Geita, Masoko mengine matatu ya Dhahabu yamefunguliwa katika Kijiji cha Nyakagwe pamoja na Kata za Nyarugusu na Katoro ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Mratibu wa ufunguaji wa Masoko hayo ya dhahabu ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema mpango uliopo ni kufungua masoko 9 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa, ambayo dhahabu hupatikana kwa wingi.
Mhandisi Robert amesema lengo la kufungua masoko hayo ni kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli katika kudhibiti utoroshwaji wa dhahabu na kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwenye sekta ya madini, hata hivyo ndani ya miezi 2 toka kufunguliwa kwa soko la dhahabu mjini Geita, mkoa umeweza kupokea kilo 200 kutoka kwa wachimbaji wadogo pia unatarajia kupokea kilo 400 zaidi za dhahabu.
“masoko haya ya dhahabu hayaleti faida kwa Serikali tu bali yatawasaidia hata ninyi wachimbaji wadogo, mwenye gramu moja atauza hapa na kupatiwa stahiki zake bila kuulizwa ametoa wapi dhahabu, hivyo naendelea kusisitiza hakuna mtu kuuza dhahabu nje ya masoko haya pia natoa mwezi mmoja kwa wamiliki wa illusion plant kufunga CCTV Camera ili mchimbaji anapoleta dhahabu yake aone kinachoendelea, maana nina taarifa za uwizi unaofanyika huko”amesema Mhandisi Robert.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Geita Ali Kidwaka amesema awali makusanyo ya madini mengi yalikuwa yanaenda kwenye maeneo mengine, lakini ujio wa masoko hayo yatasababisha makusanyo yote kuingia katika Halmashauri ya Wilaya.
Aidha amewataka wachimbaji wa dhahabu kulipa kodi ili iweze kusaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hususani kwenye afya, elimu, maji na Barabara.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa