Na Hendrick Msangi
WATENDAJI wa Kata Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Januari 05, 2024 wamekabidhiwa pikipiki kwa ajili ya kuwawezesha katika shughuli zao za kila siku katika halmashauri ya wilaya ya Geita.
Akikabidhi pikipiki hizo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe Zephania Milimo Masele ambaye ni diwani wa kata ya Nzera yalipo makao makuu ya Halmashauri amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa bidii kwa kuwatumikia wananchi.
Zephania Milimo Masele Diwani wa kata ya Nzera wa kwanza kushoto akisoma nyaraka wakati wa kukabidhi pikipiki 23 zilizotolewa kwa Watendaji wa kata
“Mkafanye kazi kwa bidii mkawahudumie wananchi na sio kuzitumia pikipiki mlizopewa katika biashara ya bodaboda, pia mzitunze na kuwa waangalifu mnapozitumia, pikipiki hizi zikawasaidie kufanya majukumu yenu ya kila siku na muweze kufika kwenye matukio kwa wakati kutekeleza majukumu yenu” alisema Masele
Aidha Diwani huyo alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha mazingira mazuri kwa watumishi ili kuendelea kuwatumikia wananchi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Sara Yohana amesema pikipiki hizo ambazo watendaji wamekabidhiwa zimenunuliwa kutokana na mapato ya ndani ambapo amewetaka watendaji hao kuzitumia katika shughuli za ukusanyaji wa mapato na kazi nyingine za kiutendaji katika maeneo yao.
Bi Sara Yohana Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wa pili kushoto akisoma taarifa ya awali kwa watumishi wa Halmashauri na watendaji wa kata wakati wa kukabidhi pikipiki 23 zilizotolewa kwa Watendaji wa kata Leo Januari 5, 2024.
“Jumla ya Pikipiki zilizokabidhiwa ni 23 zenye thamani ya shilingi 72,709,100 kutoka mapato ya ndani, awali zilitolewa pikipiki 9 ambazo zilitoka serikali kuu na tayari watendaji walishapewa hivyo halmashauri katika bajeti zake itatenga kiasi kingine cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa pikipiki 5 ili kukamilisha jumla ya pikipiki 37.” Alisema Kaimu Mkurugenzi
Akitoa shukrani kwa niaba ya watendaji wa kata ndugu Lusekelo Mwaikanda ambaye ni mtendaji wa kata ya Nyarugusu ameishukuru ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kuwawezesha watendaji wa kata kupata pikipiki hizo ili ziweze kuwasaidia kutekeleza majukumu yao. “Kwa niaba ya watendaji tunashukuru kupewa pikipiki hizi na tutazitunza, hazitatumika kwa ajili ya biashara, sisi watendaji ni nguvu ya Taifa” alisema Mwaikando.
Ndugu Lusekelo Mwaikenda Mtendaji wa kata ya Nyarugusu akiwa kwenye Moja ya pikipiki zilizotolewa leo Januari 5, 2024 Kwa Watendaji wa Kata
Zoezi hilo la ugawaji wa pikipiki limeshuhudiwa na Mhe Mbunge wa Jimbo la Busanda Mhandisi Tumaini Magesa ,Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Halmashauri ya wilaya ya Geita pamoja Watendaji wa kata za Halmashauri hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongoza na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi ili kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa wananchi ikiwa ni pamoja na ukamilishwaji wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa