Na Michael Kashinde
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Barnabas Mapande amewataka wahandisi wanaosimamia miradi mbalimbali ya Serikali kuongeza umakini katika usimamizi wa miradi hiyo kwa kudhibiti kasoro mbalimbali zinazoweza kujitokeza ili ubora wa miradi hiyo uendane na thamani halisi ya fedha inayotumika.
Ametoa wito huo Agosti 11 akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati ya Siasa Wilaya katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo wajumbe hao wamepongeza hatua za miradi mbalimbali waliyoitembelea katika siku ya kwanza ya ziara hiyo.
Ziara ya wajumbe wa kamati ya Siasa Wilaya imeanzia katika kata ya Izumacheli kwa kutembelea Mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Izumacheli pamoja na mradi wa maji unaosimamiwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA).
Aidha baada ya ukaguzi wa Miradi hiyo wajumbe hao wakiongozwa na mwenyekiti Mapande wameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kusogeza huduma hizo za kijamii kwa mara ya kwanza katika maeneo hayo ya kisiwani ambayo yalikuwa yanakabiliwa na uhaba wa maji na ukosefu wa shule kwa muda mrefu, huku akitoa wito kwa RUWASA kumfuatilia kwa karibu Mkandarasi wa maji ili amalize mradi kwa wakati sanjari na kuwasiliana kwa karibu na wadau wanaojitolea katika ujenzi wa shule ya sekondari Izumacheli ili Mradi huo wa madarasa ukamilike.
Majuto Cleophace Baltazari mmoja wa wananchi wa Izumacheli amesema kuwa uwepo wa Shule hiyo umewapunguzia gharama ambazo awali walikuwa wakitumia kuwapangishia vyumba wanafunzi wanaokuwa wanasoma mbali hasa Nkome kwa kuwa hakukuwa na shule ya sekondari kabla katika kisiwa hicho.
Wajumbe hao wametembelea pia Mradi wa Zahanati na nyumba ya watumishi katika kijiji cha Chelameno kata ya Lubanga ambao mpaka sasa umegharimu kiasi cha Tshs.108,263,480/= ambapo licha ya kupongeza ujenzi wa mradi huo Mwenyekiti Mapande ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Geita kumsaidia mtendaji wa kijiji hicho kutoa fedha kwenye akaunti ya kijiji kiasi cha Tshs. 50,000,000/= ili kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo kabla ya kikao cha Halmashauri kuu ya Chama Wilaya.
Aidha ziara hiyo imefika pia katika mradi wa shule mpya ya Nyanza katika kata ya Nzera unaohusisha vyumba 8 vya madarasa, utengenezaji wa meza 320, na viti 320, vyumba ya maabara, (Kemia, Fizikia, na Bailojia), jengo la utawala, Maktaba, ICT, matundu 20 ya vyoo vya wanafunzi na 4 ya walimu na mfumo wa maji.
Mpaka sasa shule mpya ya Nyanza imekamilisha vyumba vya madarasa 8 na majengo mengine yanaendelea na ukamilishaji ambapo wajumbe wa kamati ya Siasa Wilaya wameshauri kuongeza umakini ili miradi inayojengwa kwa gharama kubwa kama hii iwe na ubora unaotakiwa ili kuleta tija kama ilivyokusudiwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa