Na. Michael Kashinde
Mwenyekiti wa kamati ya Siasa Wilaya ya Geita Barnabas Mapande ametoa wito kwa viongozi mbalimbali kumsaidia Mhe. Rais Samia, kwa kusimamia vizuri fedha zinazokuja kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ili dhamira yake ya kuleta maendeleo ionekane kwenye jamii.Mapande ametoa wito huo Agosti 12, 2022 alipoambatana na wajumbe wa kamati ya Siasa Wilaya ya Geita na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali katika ziara ya siku ya pili ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita akiwa katika shule mpya ya Mama Samia Katoro inayojengwa kwa Gharama ya Tshs. 600,000,000/= kupitia Mradi wa SEQUIP.
Mapande amepongeza usimamizi mzuri wa ujenzi wa mradi huo ambao hauna kasoro, huku akiendelea kutoa wito kwa Wahandisi wanaopewa dhamana ya kusimamia miradi mbalimbali kuwaelekeza mafundi viwango vya miradi ya Serikali, ili kujenga miradi yenye ubora na itakayodumu muda mrefu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Wilson Shimo amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuleta miradi mingi katika Wilaya ya Geita, sambamba na wananchi ambao wamepokea vizuri miradi hiyo na kushiriki kwa kujitolea katika hatua mbalimbali kama vile kuchimba mawe ya msingi na kuleta maji huku akiendelea kuwasisitia wasimamizi wa miradi hiyo kuwaongoza mafundi muda wote ili kuepuka kazi kuharibika.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Busanda Mhe. Tumaini Magesa amewataka wananchi kujiandaa na miradi mbalimbali inayokuja ukiwemo mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Stamico hadi Ushirombo, ujenzi wa Chuo cha VETA katika jimbo la Busanda na kusambazwa kwa umeme katika vijiji vyote vya Busanda kwa Gharama ya shilingi bilioni 25 huku akikishukuru chama chake cha CCM kwa namna kinavyosimamia miradi ya maendeleo.
Mhe. Khadija Said ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ameshukuru kwa ushauri mzuri wanaoupata kutoka kwa viongozi mbalimbali wa chama na Serikali akiahidi kuufanyia kazi huku akishukuru pia kwa Mradi wa shule mpya hiyo ya Mama Samia ambayo anaamini itawahamasisha wanafunzi wengi hasa wa kike kuwa kama Rais wao Mama Samia.
Shule ya Sekondari Katoro imekasimishwa usimamizi wa ujenzi wa shule mpya hiyo ya Mama Samia na kuratibu matumizi ya fedha za mradi huo unaohusisha jengo la utawala, vyumba 8 vya madarasa, maktaba, chumba cha TEHAMA, maabara za kemia, fizikia, na matundu 20 ya vyoo na Tenki la juu la maji.
Agosti 11 na 12 Kamati ya Siasa Wilaya ya Geita imetembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita iliyoanza kutekelezwa kuanzia mwezi januari mwaka huu ikiwa ni ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kushauri mambo mbalimbali kulingana na namna wajumbe wa kamati walivyoona miradi hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa