Na Michael Kashinde
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita Ndg. Barnabas Mapande ametoa ushauri kwa viongozi Wilayani Geita kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo vijana wa bodaboda na waendesha bajaji na kuyahamasisha makundi hayo kujiunga na mifuko ya Bima za Afya.
Septemba 8, 2022 akiwa katika mkutano wa siku ya pili wa baraza la madiwani kwa kipindi cha robo ya nne kati ya Aprili hadi Juni 2022 katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mapande amesema kuwa vijana hao wanatakiwa kukata Bima za Afya yao suala linaloweza kuwasaidia kupata matibabu mazuri hata ikitokea mhusika amepata ajali na akawa hana fedha.
Ametoa wito kwa Halmashauri zinapokuwa zinawawezesha vijana hao kwa kuwapatia mikopo ya makundi maalumu, kuangalia namna nzuri ya kuwahamasisha vijana hao kujiunga katika mifuko ya Bima za Afya ambapo kuna utaratibu rahisi kwa makundi kama hayo kujiunga kwa kuchangia kiasi kidogo.
Ametumia nafasi hiyo kuiomba Halmashauri kuangalia namna ya kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo baadhi ya watu kwa kuambiwa Bima zao hazitumiki suala ambalo kwa sasa halitarajiwi kuendelea kujitokeza, kwa kuwa tayari fedha zilizotolewa na wanufaika wa Bima hizo zimekwishapelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya tayari kwa ajili ya kuwahudumia wanufaika hao.
Aidha Mapande ametumia nafasi hiyo pia kuwataka watumishi wa NIDA Wilayani Geita kuangalia namna ya kuwasaidia kwa haraka baadhi ya wananchi ambao mpaka sasa bado hawajapata vitambulisho wala namba zao za NIDA.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe. Charles Kazungu amewashukuru viongozi wa ngazi mbalimbali kwa namna waliyohamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya watu na makazi ambalo limekamilika kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuhesabu kaya 194,064 sawa na Asilimia 142 ya makadirio ya kufikia kaya 136,388, huku nyumba 233,957 sawa na asilimia 158 zikihesabiwa kutoka makadirio ya nyumba 148,000.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa