Serikali imetangaza rasmi kuwa kila mwaka yatafanyika maonesho ya kitaifa ya Madini Mkoani Geita, kwa kuwa ndio kitovu cha madini ya Dhahabu hapa nchini huku ikiahidi kuendelea kuboresha zaidi sekta hiyo.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa leo septemba 22, wakati akifungua rasmi maonesho ya nne ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini katika viwanja vya bombambili Geita, ambapo ameiagiza Mamlaka ya Maendeleo ya biashara Tanzania (TAN TRADE)kuyafanya Maonesho hayo kuwa ya kudumu.
Mh.Majaliwa ambaye alifungua maonesho ya kwanza kabisa ya madini mwaka 2018 amesema kuwa maonesho ya kitaifa ya madini yatakuwa yakifanyika Mkoani Geita kuanzia mwakani, huku akiagiza kuboreshwa kwa miundombinu ya maonesho hayo ikiwemo mabanda ya kudumu, sambamba na kuanza mapema utaratibu wa kuwaalika wageni kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya maonesho hayo.
Aidha Waziri Mkuu amesema pia kuwa Serikali inaendelea kutumia mbinu mbalimbali kuboresha sekta hiyo ya madini ambapo kwa sasa Serikali imeamua kufuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa madini yanayouzwa hapa nchini kutoka nje ili kukuza biashara hiyo.
Awali akitoa salamu kwa wananchi Mbunge wa jimbo la Geita Vijijini Joseph Kasheku Msukuma amesema kuwa juhudi kubwa zilifanywa na baraza la madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita katika kupata fedha kutoka kwa wawekezaji GGML ambao walikuwa wakitoa milioni 450 kwa mwaka tofauti na sasa ambapo wanatoa kiasi cha shilingi bilioni 3.4 kwa mwaka.
Maonesho hayo yameanza septemba 16 mwaka huu yakiratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, ambapo kilele chake ni septemba 26 na leo yamefunguliwa rasmi na Waziri mkuu wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa,huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ’’SEKTA YA MADINI KWA UKUAJI WA UCHUMI NA MAENDELEO YA WATU”
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa