Waganga Wafawidhi kutoka vituo vya afya pamoja na Waratibu wa Lishe Halmashauri ya wilaya ya Geita, leo May 3,2024 wamepata mafunzo kuwajengea uwezo katika maswala ya Lishe.
Awali akifungua mafunzo hayo, Dkt Esideri Nyandoto ambaye ni mratibu wa kinywa na meno Halmashauri ya wilaya ya Geita amewataka wataalam hao kuzingatia mafunzo hayo pamoja na utoaji wa taarifa sahihi katika majukumu ambayo wanatakiwa kuyatolea taarifa ikiwa ni pamoja na changamoto wanazokutana nazo katika maeneo yao ya kazi.
Mafunzo hayo yametolewa na na maafisa lishe wa Halmashauri ya wilaya ya Geita ili kuendelea kukabiliana na tatizo la utapiamlo unaotokana na lishe duni inayopelekea udumavu kwa watoto.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita bi Ummy Kileo amesema upo Muongozo mpya wa makundi ya vyakula ambapo amesema kwa sasa makundi yapo sita na sio matano. Ummy ameyataja makundi hayo kuwa ni kundi la Nafaka, mizizi yenye wanga ndizi za kupikwa, kundi la mboga mboga, kundi la matunda, kundi la jamii ya kunde, karanga na mbegu zenye mafuta, kundi la vyakula vyenye asili ya wanyama na kundi la mwisho ni kundi la mafuta ambayo ni salama kwa afya.
Muuguzi Kiongozi Hospital ya Wilaya Nzera, Beatrice Munisi amewataka waganga Wafawidhi na maafisa lishe wa vituo vya afya kuwa huduma zenye utu, staa na Heshima katika kutoa huduma huku akiwataka kuwa na mahusiano mazuri ya kuheshimiana nakupenda katika kufanya kazi ili wateja waendelee kupata Huduma Bora.
Aidha katika mafunzo hayo, wataalam hao wamejifunza namna ya kufanya utambuzi wa watoto wenye utapiamlo wa kadiri na mkali kwa kutumia vigezo vya shirika la Afya duniani (WHO) ambapo imeelezwa kwa mujibu wa vigezo vya shirika la Afya duniani (WHO) utapiamlo wa kadiri kwa watoto unamaanisha uwiano wa uzito kwa urefu kati ya Z-alama (mstari wa ukuaji)-3 na <-2 (bila kivimba mwili) , au mzingo wa kati wa sehemu ya juu ya mkono chini ya sentimeta 12.5 lakini ni sawa au zaidi ya sentimeta 11.5.
Kwa upande wa utapiamlo mkali kwa watoto wenye umri kuanzia miezi 6 hadi 59 hutokanana na lishe duni inayojidhihirisha kwa ukondefu mkali wa mwili , ambapo uwiano wa Uzito kwa urefu/kimo upo chini ya Z-score-3 kwenye mstari wa ukuaji au kuvimba kwa miguu yote miwili, au mzingo wa kati wa sehemu ya juu ya mkono chini ya sentimeta 11.5.
Katika mafunzo hayo, Waganga Wafawidhi pamoja na Waratibu wa Lishe katika vituo vya afya ndani ya Halmashauri wametakiwa kuwaelemisha wazazi na walezi wa watoto kula vyakula mchanganyiko kutoka makundi sita ya chakula kila siku kwa na kuzingatia tofauti za vyakula ndani ya kila kundi ili kuzuia utapiamlo na kupunguza hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyoambukizwa.
Dkt Jumanne Enos akitoa mafunzo kwa waganga Wafawidhi na Maafisa lishe kutoka vituo vya afya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo amewataka waganga hao na maafisa Lishe kuwashauri wamama wanapojifungua kupata vyakula vya Lishe ili kutengeneza maziwa mengi kwa ajili ya watoto.
Pamoja na hayo, wametakiwa kutoa elimu kwa wazazi na walezi wanao fika kwenye vituo vya afya kuhakikisha wanazingatia usafi wa mazingira katika maeneo wanavyoishi na Usalama wa chakula na maji ikiwa ni pamoja na kuepuka tabia hatarishi za matumizi ya sigara, tumbaku na unywaji wa pombe ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa kwa kuwa na mtindo bora wa maisha.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Waratibu wa Huduma za mama na mtoto, Wauguzi na maafisa lishe ndani ya Halmashauri ambapo kwa nyakati tofauti wamewataka washiriki wa mafunzo hayo kufikisha elimu katika ngazi zote katika vituo vyao vya kazi ili kuendelea kuwajengea uwezo katika kukabiliana na maswala ya Lishe.A
Halmashauri ya Wilaya ya Geita imepokea jumla ya kiasi cha Shilingi milioni 204 kwa ajili ya huduma za afua za lishe katika vituo 57 vya kutoa huduma za Afya.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa