Dodoma, Januari 29, 2025 – Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wamehudhuria mafunzo maalum kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) Hombolo, Dodoma, kwa lengo la kuboresha utendaji wao katika halmashauri. Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku mbili, Januari 29 na 30, 2025, katika ukumbi wa African Dream Hotel, yakiratibiwa na wawezeshaji kutoka LGTI.
Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakiwa katika mafunzo.
Ziara hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Charles Kazungu, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndugu Karia Magaro. Akifungua rasmi mafunzo hayo, Mhe. Kazungu alisisitiza umuhimu wa madiwani kuwa na uelewa wa kina kuhusu uongozi bora, usimamizi wa fedha, na uendeshaji wa vikao kwa ufanisi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu, akizungumza na madiwani, katika ufunguzi wa mafunzo kwa madiwani yanayoendelea Dodoma.
Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Magreth Bushesha, aliwahimiza madiwani kutumia mafunzo hayo kuboresha utendaji wa halmashauri zao. "Kuna mambo madogo kama uendeshaji wa vikao, ubunifu wa miradi, na usimamizi wa maendeleo ya jamii, ambayo yanaweza kuonekana yasiyo na uzito, lakini yanaathiri sana utendaji wa halmashauri. Ni muhimu kuyafahamu na kuyasimamia kwa ufanisi," alisema Prof. Bushesha.
Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Magreth Bushesha, akizungumza na Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita katika mafunzo yanayoendelea Dodoma.
Kwa upande wake, Dkt. Rogers Rugeiyamu, mhadhiri na mwezeshaji wa mafunzo, alibainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza tija katika halmashauri kwa kuimarisha usimamizi wa fedha na ubunifu wa vyanzo vya mapato. "Mafunzo haya yataisaidia halmashauri kuwa na mipango mizuri ya maendeleo na kujitegemea kifedha," alisema Rugeiyamu.
CPA Charles Matekele, mhadhiri wa fedha na uhasibu kutoka LGTI, alisema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha madiwani kuimarisha usimamizi wa fedha, kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali, na kupunguza hoja za kikaguzi zinazotokana na kutofuata sheria, kanuni, na taratibu.
Dkt. Rogers Rugeiyamu, mhadhiri na mwezeshaji wa mafunzo akifundisha mada katika mafunzo yanayofanyika Dodoma
CPA Charles Matekele, mhadhiri wa fedha na uhasibu kutoka LGTI akifundisha mada katika mafunzo yanayofanyika jijini Dodoma
Kwa upande mwengine , Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Karia Magaro, alitoa wito kwa madiwani kuzingatia mafunzo hayo na kuyatumia kwa vitendo. "Lazima tuhimize utaratibu wa vikao wenye tija, tuongeze mapato ya halmashauri, na kubuni miradi ya maendeleo ili kutoa huduma bora kwa wananchi wetu," alisema Magaro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Karia Magaro akizungumza jambo wakati wa uchangiaji baada ya mada, katika mafunzo yanayofanyika Dodoma
Madiwani walioshiriki mafunzo hayo walielezea manufaa yake kwa utendaji wao. Diwani wa Kata ya Ludete, Mhe. Maumuna Bulilo, alisema kuwa amejifunza mbinu mpya za kuendesha vikao kwa muda mfupi lakini kwa ufanisi zaidi. "Awali tulikuwa tukikaa vikao kwa muda mrefu, lakini sasa tumejifunza namna ya kumaliza kikao kwa saa mbili pekee bila kupoteza muda," alisema Bulilo.
Naye Diwani wa Kata ya Bukoli, Mhe. Faraj Seif, alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuboresha uendeshaji wa baraza la halmashauri, usimamizi wa fedha, uibuaji wa miradi, na ushirikiano na wananchi.
Akihitimisha mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Charles Kazungu, alitoa wito kwa madiwani kuyatumia mafunzo hayo kwa maendeleo ya halmashauri na jamii kwa ujumla. "Mafunzo haya yakalete chanya si tu kwa halmashauri lakini pia kwa jamii tunayoiongoza. Yakalete chanya katika usimamizi wa miradi, usimamizi wa fedha, na pia katika kuelimisha wananchi namna ya kulipa kodi pamoja na tozo za halmashauri ili halmashauri iweze kuendeshwa kwa ufanisi," alisema Kazungu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa