Na Hendrick Msangi
Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita sambamba na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashuri hiyo wamefanya ziara katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Novemba 23, lengo kuu ikiwa ni kujifunza namna ya uendeshaji wa shughuli za maendeleo na kubadilishana uzoefu katika utendaji.
Awali akiwakaribisha Waheshimiwa Madiwani, Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama ndugu Clemence Mkuja aliwaeleza Waheshiwa Madiwani na Wakuu wa Idara na Vitengo namna ambavyo Manispaa hiyo inaendesha shughuli zake na kupata mafanikio makubwa katika miradi ambayo inaendelea katika manispaa hiyo ikiwa ni pamoja na utaratibu wa vikao vya baraza kufanyika kwa muda mfupi.
Akiendelea kutoa uzoefu kwa Waheshimiwa Madiwani na Wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wa namna wanavyosimamia miradi, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema, Menejimenti inapofanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao huleta ufanisi mzuri katika utekelezaji wa miradi wanayokuwa nayo. “Menejimenti hukubaliana kufanya miradi michache katika mwaka wa fedha na kukubaliana na waheshimiwa madiwani kuwa miradi ni kwa ajili ya Manispaa na sio Kata jambo ambalo hupelekea kufanya miradi michache na inayokamilika kwa ufanisi na ubora kwa kuzingatia fedha iliyotengwa” alisema Mkuja.
Pamoja na hayo, Manispaa hiyo huweka vipaumbele vya miradi inayotekelezwa kwa mwaka wa fedha na kuwa na miradi ya kimkakati ambayo hushirikiana na wataalam katika kuiandaa.
Waheshimiwa Madiwani na Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakisikiliza namna Manispaa ya Kahama wanavyoendesha Shughulizi za Hospitali ya Manispaa hiyo inayohudumia wagonjwa ndani na nje ya Manispaa hiyo.
Kwa upande wa uwekezaji Manispaa ya Kahama yenye jumla ya kata 20 ,alisema wanatoa ardhi bure kwa wawekezaji ambapo menejimenti hukaa na kamati husika kisha hupeleka kwenye baraza la madiwani na kufanya maamuzi ya pamoja kwa kutoa ardhi bure kwa ajili ya uwekezaji. “Halmashauri ya Manispaa ya Kahama hutoa ardhi bure kwa ajili ya uwekezaji lengo kubwa ni kutengeneza na kuzalisha ajira nyingi kwa wananchi wa Kahama kupitia wawekezaji wanaokuja kuchukua ardhi ambayo hutengwa kwa kuzingatia sheria za ardhi” alisema Kaimu Mkuregenzi huyo.
Madiwani na Wakuu wa Idara wakiwa kwenye Moja ya eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanda kwa wawekezaji ambalo limetolewa bure ili kuwavutia wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza na kuzalisha ajira nyingi kwa wakazi wa Kahama.
Sambamba na hilo, Halmashauri hiyo hutoa ajira za muda mfupi katika ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kuwa na wiki ya ukusanyaji wa mapato ambapo Wakuu wa Idara na Vitengo huingia mtaani kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa mapato kwenye manispaa hiyo na kuweza kutenga fedha kupitia mapato ya ndani kuwawezesha wajasiriamali pamoja na kuhamasisha vijana kwenye sekta ya kilimo na kuongeza ajira.
Waheshimiwa Madiwani na Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakiwa kwenye moja ya kumbi ndogo za mikutano za Manispaa hiyo ambayo samani zake zimetengenezwa na wajasiriamali wa Manispaa hiyo. Samani zinazotumika kwenye ofisi za Manispaa hiyo hutengenezwa na wajasiramali wa Manispaa hiyo ikiwa ni sehemu ya kuendelea kutengeneza ajira nyingi kwa vijana.
Naye Kaimu Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Mzee Hamidu Kapamwa aliwaasa madiwani hao kutokuwa na uadui na watendaji wa halmashauri yao bali kuwa kitu kimoja kwa kufanya kazi kwa kushirikishana , kuheshimiana , kupendana na kuzungumza lugha moja na kwenda pamoja ili kuleta maendeleo katika halmashauri yao.
Moja ya Kiwanda cha samani ambacho Manispaa ya Kahama imetoa eneo bure (Ummy Mwalimu Industrial) kwa ajili ya mradi huo ambao zinatengenezwa samani mbalimbali zinazouzwa ndani na nje ya nchi na kuiongezea Manispaa hiyo mapato ya ndani.
Madiwani hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshima Charles Kazungu waliwashukuru wenzao wa Manispaa ya Kahama kwa ukarimu na mapokezi mazuri waliyoyapata na kuwa ahidi kuyafanyia kazi yote waliyojifunza wakishirikana na wataalam ili kuleta maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kutumia uzoefu waliojengewa na wenzao na kuwaomba wazidi kuwa marafiki ili kuendelea kushirikishana namna ya kuendelea kuzijenga Halmashauri ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri wa miradi ambayo serikali inayo ongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa