Na Hendrick Msangi
Maafisa Habari nchini wametakiwa kutumia taaluma yao kuelimisha jamii umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza inayotarajiwa kuanza Julai 1 , 2024.
Akizungumza katika Kikao cha Tume huru ya Uchaguzi na Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri kilichofanyika Ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi Ndugu Ramadhani Kailima amewataka Maafisa Habari wa Serikali Kuwa mabalozi wazuri wa Tume huru ya Uchaguzi kwa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ndugu Ramadhani Kailima akizungumza katika Mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Maafisa Habari kutoka Mikoa na Halmashauri nchini Katika Ukumbi wa Mliman City Jijini Dar es Salaam Juni 15,2024.
Hayo yameelezwa Juni 15, 2024 wakati wa Mkutano wa Tume Huru ya Uchaguzi na Maafisa Habari kote nchini.
"Ndugu Maafisa Habari, uboreshaji huu unahusu kila mwananchi mwenye sifa, Tumieni njia mbalimbali kuelimisha jamii umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza" Amesema Ndg Kailima.
Awali akiwasilisha mada kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Kwanza, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura Bi. Giveness Aswile amesema zoezi hilo linatarajia kuzinduliwa Julai 01, 2024 katika Mkoa wa Kigoma na kisha kuendelea katika mikoa mingine ya Katavi na Tabora, na kufuatiwa na Kagera na Geita na kasema zoezi hilo hadi kufika Machi 2025 zoezi hilo linatarajiwa kukamilikana kwa awamu ya kwanza.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura Bi.Giveness Aswile akizungumza katika Mkutano huo ambapo amesema Kada ya Maafisa Habari ni muhimu kwa nchi yoyote inayotaka kufanikisha Jambo la aina yoyote .
Pamoja na hayo Bi Givennes amebainisha kuwa baada ya uboreshaji wa daftari hilo inatarajiwa kuwa jumla ya wapiga kura 34,746,638 watakuwa wameandikishwa.
“Katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Daftari linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638 kutoka 29,754,699 ya mwaka 2020 hili ni ongezeko la wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7,” amesema Bi. Givennes katika Mkutano huo.
Aidha Bi Givennes ameongeza kuwa katika zoezi hilo wapiga kura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wataondolewa katika Daftari kwa kupoteza sifa za kuwa wapiga kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 10 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na 1 ya mwaka 2024.
Akizungumzia kuhusu mfumo mpya saidizi unaofahamika kama Online Voters Registration System, (OVRS) amesema mfumo huu utawawezesha wapiga kura walioandikishwa kuanzisha mchakato wa uboreshaji kwa njia ya mtandao kupitia simu ya mkononi au Kompyuta kubadilisha taarifa au kuhama jimbo au kata au kubadilisha na kuhama.
Maafisa Habari kutoka Mikoa na Halmashauri nchini Tanzania wakifuatilia mada kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga Kura awamu ya kwanza ndani ya Ukumbi wa mikutano wa Mliman City Jijini Dar es Salaam.
Jumla ya vituo 40,126 vya kuandikisha wapiga kura vitatumika katika uboreshaji wa Daftari 2024 ambapo 39,709 vipo Tanzania Bara na 417 vikiwa Zanzibar nakufanya Tume kuwa na ongezeko la vituo 2,312 kulinganisha na vituo 37,814 vilivyotumika mwaka 2019/2020.
Kauli mbiu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania inasema Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni Msingi wa Uchaguzi bora
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa