Na Michael Kashinde
Kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 8, kila mwaka Halmashauri ya Wilaya ya Geita imewaunganisha wadau mbalimbali wa masuala ya wanawake, na kushiriki kwa pamoja katika zoezi la kufanya usafi katika kituo cha Afya katoro sambamba na kutoa zawadi mbalimbali kwa akina mama waliojifungua pamoja na wafungwa wanawake katika gereza la Wilaya Geita.
Mazoezi hayo yaliyoratibiwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Geita yamefanyika Machi 6, 2023 yakiwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo kampuni ya dhahabu ya BUCKREEF, chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Geita (TALGWU), vikundi mbalimbali vya wanawake na Taasisi zinazojihusisha na haki za wanawake na kupinga ukatili.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Geita Bi. Enedy Mwanakatwe amewashukuru wadau hao kwa ushiriki wao katika zoezi hilo la usafi na zawadi mbalimbali walizojitolea huku akisema kuwa zawadi hizo zitawasaidia akina Mama hao pamoja na watoto wao.
Zawadi hizo ni pamoja na Sabuni katoni 25, Sukari kilo 160, madaftari(Counter books) boksi 12, sabuni za Detol boksi 2 kutoka Kampuni ya BUCKREEF, huku chama cha wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Geita (TALGWU) wakitoa Taulo za kike kubwa pisi 174 Taulo kwa ajili ya watoto (Pumpers)Pisi 288 na Gloves boksi 3.
Bi. Amelda Msuya Meneja rasilimali watu katika mgodi wa dhahabu wa BUCKREEF akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo amesema kuwa, wameona ni vyema kushiriki na wanawake katika mwezi huu kwa kuwa na wao kama mgodi wana sera ya kuajiri wanawake wengi kadri wawezavyo ili kuendelea kuwatia moyo wanawake kufanya shughuli za madini ambapo hapo awali jamii iliamini shughuli za migodini zinafanywa na wanaume pekee jambo ambalo kwa sasa limebadilika.
Kwa upande wake Katibu wa TALGWU mkoa wa Geita Wakili Daud Mhagama amesema kuwa wao kama chama cha wafanyakazi wamejitokeza kuungana na wadau wengine kushiriki katika zoezi hilo ili kuwaunga mkono akina mama katika shughuli zao za maendeleo akiwemo Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mama.
Akizungumza pia baada ya kupokea zawadi mbalimbali zilizotolewa kwa ajili ya wafungwa na mahabusu wanawake, katika gereza la Wilaya ya Geita Mratibu Msaidizi wa Magereza Samwel Evans Juma awashukuru wanawake hao kwa zawadi hizo akisema kuwa hiyo inaonyesha wazi kuwa wafungwa na mahabusu hawajatengwa na jamii na wanapotembelewa na watu wanafurahi kwa kuona jamii inawajali na kuwathamini.
Siku ya wanawake huadhimishwa duniani kote Machi 8 kila mwaka ambapo kwa mwaka huu 2023 maadhimisho hayo kwa upande wa Mkoa wa Geita yataadhimishwa kimkoa katika viwanja vya AIC Ludete ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mrtin Shigela.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa