Hii ni Kauli Mbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo kwenye Halmshauri ya Wilaya ya Geita iliadhimishwa kwenye Kata ya Kakubilo Shuleni Kawawa tarehe 16.06.2018 ikihudhuliwa na wakazi, wazazi pamoja na watoto wa eneo hilo.
Wakisoma risala yao kwa mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw. January Bikuba, watoto walilisitiza kuwa wao kama wawakilishi wa watoto wa Wilaya ya Geita wanaona maadhimisho hayo ni muhimu kwao, kwani huamini kuwa jamii ya Tanzania na viongozi kwa ujumla hutumia maadhimisho hayo katika kutafakari masuala mbalimbali ya watoto na haki zao katika kujenga taifa la leo na lijalo tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda.
Walisema “bado tunayo huzuni kutokana na Ukatili na Unyanyasaji kimwili, na kijinsia pamoja na mimba za utotoni tungali wanafunzi hali inayotupelekea kushindwa kujiamini, kufifisha na kuua ndoto zetu katika maisha, yote haya yanayosababishwa na mazingira hatarishi tunayoishi, baadhi ya wazazi na walezi ambao hushinikiza waoto kuacha shule na kujitika kwenye biashara ndogondogo ili kujipatia fedha za kujikimu” walimaliza. Hivyo ombi lao kwa serikali na wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari Kuelekea Uchumi wa Viwanda ni kupaza sauti kwa umma juu ya kujali haki za watoto.
Akiongea na wazazi na walezi wa watoto wa Kata hiyo, Bw. Bikuba aliwashukuru wananchi hao kwa mahudhurio na maandalizi mazuri ya watoto ambapo alijionea burudani mbalimbali za ngoma, kwaya na mashairi kutoka kwa wanafunzi wa shule za msingi Kawawa, Kabayole na Kakubilo bila kusahau mechi ya mpira kati ya shule ya sekondari ya Senga na Kakubilo.
“kutokana na changamoto za upungufu wa miundombinu ya elimu, bado siri ya mafanikio ni wananchi kujitolea kutekeleza shughuli za maendeleo katika sekta mbalimbali mfano elimu na afya kwa kusomba mawe, kokoto, kufyatua na kuchoma tofali n.k ili kumwekea mtoto mazingira mazuri” bw. Bikuba alisema. Aliongeza kwa kusema, Serikali itachukua hatua mbalimbali za kisheria kwa wale watakaobainika kuwapatia mimba watoto wa kike na wazazi wanaowaozesha wanafunzi katika umri mdogo bila kuwasahau walawiti na wabakaji. Lakini pia aliwaasa wazazi waendelee kuwalea watoto katika maadili mema na kuwapa haki zao za msingi.
Mwisho mgeni rasmi alikabidhi zawadi zikiwemo kalamu, madaftali na mipira ya miguu kwa watoto walioshiriki maadhimisho na michezo mbalimbali. Sherehe hizo ziliandaliwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na ofisi Kata ya Kakubilo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa