Na. Michael Kashinde
Katika Kuadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Cornel LG Magembe ametoa wito wa kuendelea kuhifadhi mazingira kwa kupanda angalau miche mitano kwa kila familia, hali itakayoendelea kuhifadhi na kutunza mazingira yao ambayo kwa sasa ni kichocheo kizuri cha shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo na ufugaji.
DC Magembe ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya Nyamboge Aprili 25, 2023 katika maadhimisho ya kuelekea miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyoambatana na sherehe za uzinduzi wa zahanati ya Chelameno na Nyumba ya Mtumishi (Two in One), pamoja na zoezi la kupanda miti katika eneo la zahanati hiyo ambapo amesisitiza uhifadhi wa mazingira ili kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji mbalimbali katika familia.
DC Magembe ameisifu hali ya hewa ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambayo inawawezesha wakulima kuvuna mahindi kwa awamu mbili huku akiwataka kuendelea kutunza hali hiyo kwa kudhibiti uharibifu wa mazingira akiwasisitiza kuendelea kujituma kuchapa kazi ili kuongeza kipato na kuwahakikishia kuwa Serikali yao itaendelea kuwaletea huduma za Msingi za kijamii kama vile barabara, maji, Afya na Elimu.
Aidha DC Magembe akiwa miongoni mwa watu waliowahi kuishi katika kata ya Nyamboge miaka ya nyuma akiwa mwanafunzi ameisifu kazi iliyofanyika katika kipindi chote hiki cha miaka 59 ya Muungano kwa kusema kuwa miundombinu ya barabara, Afya na Elimu imeboreshwa sana tofauti na zamani ambapo walikuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda shuleni huku akieleza kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya kuboresha na kurahisisha huduma za kijamii ili kuleta maendeleo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM Wilaya ya Geita Ndg. Timothy Sanga akizungumza na wananchi hao amesema kuwa wao kama Chama Cha Mapinduzi wanaamini kuwa watu wakiwa na Afya bora nchi inapata maendeleo, hivyo kwa miaka 59 ya Muungano chama kimeendelea kuwa bora na kuisimamia Serikali katika kutekeleza Ilani ya CCM.
Aidha ametoa wito kwa wataalamu watakaoishi katika nyumba hizo za watumishi kuwahudumia wananchi hao kwa moyo wa upendo, umoja, amani na utulivu kwa kuwa wakipata huduma bora wataisifu Serikali na wakipata huduma mbovu wataisema vibaya Serikali ambayo dhamira yake ni kuona wananchi wanapata huduma bora za kijamii.
Awali akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Wakili Msomi John Wanga amesema kuwa mpaka sasa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina hospitali mbili zenye hadhi ya Wilaya ambazo ni hospitali ya Katoro na Nzera ambazo zinaendelea kuwahudumia wananchi.
Wanga ameendelea kumshukuru Mhe. Rais Mama Samia kwa kuwajali wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo kwa kipindi cha miaka miwili amewapatia zaidi ya kiasi cha shilingi Bilioni 7.3 kwa ajili ya miradi mbalimbali katika Sekta ya Afya.
Aidha katika kuwawezesha wananchi kiuchumi Halmashauri ya Wilaya ya Geita imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 1, milioni 197 na laki 3 bila riba kwa vikundi 98 kutoka makundi ya vijana, wanawake pamoja na walemavu.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Chelameno ndg. Hakeem Teranga na Bi. Nabayongo wakizungumzia uzinduzi wa mradi huo wa zahanati na nyumba ya mtumishi Chelameno wameishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma hiyo karibu tofauti na zamani ambapo walilazimika kusafiri kwenda hopitali ya Nzera kwa ajili ya huduma za matibabu.
Bi.Nabayongo anasema kuwa walilazimika kusafiri kwa pikipiki (bodaboda) kwa gharama ya shilingi elfu 5 kwenda au kurudi ingawa changamoto ilikuwa nyakati za usiku ambapo gharama za usafiri zilikuwa zinapanda na kuwa shilingi elfu 10 lakini pia mara nyingi walirudi nyumbani nyakati za usiku kwa kuwa walikuta foleni kubwa za wagonjwa wanapokwenda kutibiwa hospitali ya Nzera.
Maadhimisho haya ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yamefanyika katika kijiji cha Chelameno kata ya Nyamboge Halmashauri ya Wilaya ya Geita yakiongozwa na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo ” Miaka 59 ya Muungano Umoja na Mshikamano ndiyo nguzo ya kukuza uchumi wetu” yakienda sambamba na uzinduzi wa nyumba ya mtumishi (two in One) katika zahanati ya Chelameno iliyojengwa kwa gharama ya kiasi cha jumla Tshs. 100,865,712/= ambapo 10% ya pesa hiyo ni michango ya nguvu za wananchi ambayo ni 10,985,000/= huku 90% ya fedha hiyo ya mradi ilitolewa mfuko wa maendeleo ya (TASAF) kiasi cha Tshs. 89,880,712/=
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa