Na Hendrick Msangi
Katika kutimiza dhamira ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha kero zinazowakabili zinapata mwarobaini, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita imeendelea kufanya ziara kwa ajili ya Kusikiliza na Kutatua Kero za Wananchi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Akizungumza na wananchi wa kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Geita zikiwemo kata za Katoro,Ludete na Kakubilo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Martine Shigella amesema Serikali ya awamu ya sita inafanya kazi kwa kuwajibika kuwafuata wananchi ili kutatua kero ambazo zinawapata. “Serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan ni ya wananchi, hivyo kila mtendaji anawajibu wa kuwatumikia wananchi” alisema Shigella.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Martine Shigella akitatua kero za wananchi waliofika kwenye Kliniki ya kutatua kero za wananchi Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Aidha Shigella aliwataka wananchi hao kuepuka kutoa rushwa kwa watendaji wa ngazi zote pale wanapohitajika kutoa, na iwapo kutakuwa na uhitaji wa kutoa fedha basi kuwe na utaratibu katika maandishi
Kwa upande wa kero zinazohusu maswala ya ardhi, Mhe Shigella aliiagiza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuchukua hatua za haraka kwa watu wenye viwanja ambavyo wanahitaji kujenga ili kuwa na vibali kuepuka kuja kuvunja nyumba za wananchi. Akitolea mfano mji mdogo wa Katoro ambao unakuwa kwa kasi kutokana na kuwa na wafanyabiashara wengi, Mhe Shigella aliwataka viongozi wa vijiji na vitongoji kusimamia vizuri swala la ujenzi ili mji huo upangike vizuri. “Kila mtu anayetaka kujenga ni vema kushirikisha wataalam kwa ajili ya kuwa na mji uliopangika wananchi wajenge kwa kufuata utaratibu.” Alisema Mhe Shigella
Kuhusu swala la vitambulisho vya NIDA ambavyo vimeonekana kuwa kero kwa watu wengi, Mkuu huyo wa Mkoa aliagiza mamlaka zote zinazohusika katika upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA kuweka kambi maeneo ambayo wananchi hawajapata Vitambulisho ili vitambulisho hivyo vipatikane kwa uharaka.
Aidha katika kliniki hiyo wananchi walililamikia jeshi la polisi kwa kuwanyanyasa wananchi wanaobeba magunia ya mkaa kwa kuwatoza kiasi cha shilingi laki mbili ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita Kamanda Sofia Jongo alilikemea jambo hilo na kusema askari polisi wote wanajihusisha na maswala ya rushwa watachukuliwa hatua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Sofia Jongo amewataka wananchi Mkoani Geita kujiepusha na vitendo vya rushwa na badala yake watoe taarifa kwa vyombo husika pale wanapotakiwa kufanya hivyo
Pamoja na hayo zipo kero za wafanyabiasha kusumbuana na mwenyekiti wa wafanyabiasha katoro kuhusiana na mikataba ya upangishwaji wa vyumba vya biashara na ulipaji wa mapato ambapo Mkuu wa mkoa aliagiza wafanyabiashara hao kuendelea kulipa Halmashauri kama wapangaji wa Halmashauri.
Kuhusu migogoro kati ya wamiliki wa mashamba ambayo yamegundulika kuwa na miamba ya madini na wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini kutokutoa asilimia 10 kwa wamiliki wa mashamba hayo, Mkuu wa Mkoa aliagiza wanaotaka kuchimba madini waelewane na wananchi wanaomiliki ardhi ili kuepuka migogoro.
Kuhusu michango wanayochangishwa wanafunzi shuleni, Mhe Mkuu wa Mkoa aliagiza michango hiyo kufuata kibali maalumu kutoka kwa mkuu wa wilaya ili kuepuka migogoro na kusema watoto wasirudishwe nyumbani na kukosa masomo bali utaratibu ufuatwe.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Mkoa wa Geita ambapo walisikilizwa kero zao na kupatiwa ufumbuzi. Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan inawafikia wananchi kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Aidha katika ziara hiyo kuliibuka kero kutoka kwa wananchi kuhusu kituo cha afya kakubilo kukamilika muda mrefu lakini hakitoi huduma hivyo kumlazimu Mbunge wa jimbo la Geita vijijini Mhe Joseph Msukuma kutolea majibu mbele ya wananchi na mkuu wa mkoa.
Kufuatia maombi hayo ya wananchi na mbunge ya kufunguliwa kwa kituo hicho cha afya, Mkuu wa Mkoa Wa Geita Mhe Martin Shigella alimuagiza Mganga Mkuu wa wilaya kukifungua mara moja kituo hicho na kuanza kutoa huduma wakati ukamilishaji wa majengo mengine ukiendelea.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Mkoa wa Geita ambapo walisikilizwa kero zao na kupatiwa ufumbuzi. Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan inawafikia wananchi kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Akihitimisha ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa Mhe Martine Shigella aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza na kuwasihi kufika kwenye ofisi za umma kwa ajili ya utatuzi wa kero zao kwani ofisi zipo kwa ajili yao ikiwa ni pamoja na kuwapa ushirikiano viongozi wao ili kuleta maendeleo katika maneo yao huku akikemea swala la ukatili kwa watoto, rushwa na kuwasisitiza wananchi hao kutambua kuwa swala la ulinzi na usalama ni jukumu la kila mtu.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa