Na: Hendrick Msangi
IDARA ya Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Januari 9, 2024 imekutana na Maafisa Elimu Kata wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kujadili taarifa ya tathmini ya matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi uliofanyika mwaka 2023
Matokeo hayo yaliyatangazwa na baraza la mtihani Tanzania (BMT) Novemba 23, 2023 na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohammed, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilikuwa na jumla ya watahiniwa 23,335 walioshiriki kufanya mtihani huo na kushika nafasi ya 5 kati ya Halmashauri 6 za Mkoa wa Geita katika ufaulu wa watahiniwa waliofanya mtihani huo wa upimaji darasa la saba 2023.
Jumla ya shule zilizofanya mtihani huo kwa Halmashauri ya wilaya ya Geita zilikuwa 201 zikiwemo shule 5 za watu binafsi na mashirika ya dini ambapo kiwango cha ufaulu kwa mwaka 2023 ni asilimia 69.65 hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.1 za ufaulu kulinganisha na mwaka 2022 ambapo kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 64.48.
Akizungumza katika kikao hicho cha kujadili taarifa ya tathmini ya matokeo ya mtihani huo wa upimaji katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri, Kaimu Mkuu wa Divisheni Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mwl Paul Richard Magubiki amezipongeza kata za Ludete, Katoro, Nyarugusu, Nkome na Nyamigota kwa kufanya vizuri kati ya kata 37 za Halmashauri hiyo na kuzitaka kata ambazo hazikufanya vizuri kuongeza juhudi ili kuleta matokeo mazuri kwa mitihani ijayo.
Maafisa Elimu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita katika kikao cha kujadili taarifa ya tathmini ya matokeo ya mtihani wa darasa la saba uliofanyika mwaka 2023 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilishika nafasi ya tano katika ufaulu wa mtihani huo kati ya Halmashauri 6 za Mkoa wa Geita
Aidha alieleza lengo la kikao hicho ni kujadili taarifa ya tathmini ya matokeo ya mtihani wa upimaji darasa la saba uliofanyika Septemba 13 -14 mwaka 2023 na kuweza kuweka mikakati itakayowezesha kuwa na muelekeo mzuri kwa mwaka 2024.
Pamoja na hayo Afisa Elimu huyo aliwaeleza Maafisa Elimu kata kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Imedhamiria kupandisha kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 69.65 ya mwaka 2023 hadi kufikia asilimia 85 kwa mwaka 2024 ambapo alisema ni vema kila kata kusimamia mikakati waliyojiwekeaa ili kuongeza kiwango cha ufaulu . “Mkawahimize Walimu Wakuu kuwasimamia walimu kufundisha na kufika kazini kwa wakati kwa kuendelea kuwakumbusha sheria na taratibu za utumishi ili tuweze kuitimiza kauli mbiu yetu ya Usimamizi na ufuatiliaji katika sekta ya elimu huleta matokeo chanya na halisia” alisema Magubiki.
Aliendelea kuwaeleza Maafisa Elimu kata hao kuendelea kuhimiza swala la lishe kwa wanafunzi wawapo shuleni na kuzitaka kamati za lishe kuwajibika kwani mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa ambayo haikufanya vizuri kwenye afua za lishe. Pia Afisa Elimu huyo aliwataka Maafisa Elimu kata hao kuwafuatilia wazazi wa wanafunzi watoro ili kuwachukulia hatua hii ni pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu kwa walimu wasiotimiza wajibu wao.
Maafisa Elimu kutoka kata 37 za Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakiwa kwenye kikao cha kujadili taarifa ya tathmini ya matokeo ya mtihani wa darasa la saba uliofanyika Septemba 13-14, 2023 ambapo kwa pamoja waliazimia kuweka bidii katika Usimamizi na ufuatiliaji katika sekta ya elimu ili kuleta matokeo chanya na halisia.
Jumla ya Wanafunzi 16,148 wamejiunga na elimu ya sekondari kwa mwaka wa masomo 2024 ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kumekuwa na ongezeko la shule 2 za sekondari zilizojengwa kwa fedha kiasi cha shilingi 1,168,560,056 kutoka fedha za wadau wa maendeleo kupitia serikali kuu (SEQUIP).
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za miradi ya shule zenye ubora kwa ajili ya wanafunzi wanaoendelea kufaulu na kujiunga na masomo ya elimu ya sekondari.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa