Wananchi wa kata ya Rwamgasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita wameiomba Serikali kuwasaidia kuupanua mradi wa maji uliojengwa katika kijiji cha Lwamgasa ili uweze kuwafikia wahitaji wote kwa kuwa uhitaji wa huduma hiyo ni mkubwa kutokana na idadi kubwa ya watu kwenye eneo hilo.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji wa kata hiyo Emmanuel Alphonce novemba 17, 2021 wakati akisoma taarifa ya mradi huo wa maji kwa Katibu Mkuu wa umoja wa wazazi CCM Taifa Ndg.Gilbert Kalima aliyekuwa katika ziara ya Sekretarieti ya CCM Taifa katika jimbo la Busanda.
Katika taarifa ya Ndg.Emmanuel amesema kuwa ili mradi huo uweze kuwafikia wananchi wengi wanahitaji kusaidiwa mabomba ya nchi 2 rola 17, nchi 1 na nusu rola 10, na nchi 1 rola 32 vikiwa na viungio vyake vyote 30.
Mradi huo wa maji uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 672 laki 6 na 92 elfu na 87 unawasaidia zaidi ya wananchi elfu 16 na mia 357 wa kijiji cha Lwamgasa ambao kwa sasa wanapata maji safi na salama kwa 100% kutoka 12.2% ya awali ambapo huduma ya maji ilikuwa inapatikana kutoka mradi wa zamani uliokuwa na tanki lenye ujazo wa lita elfu 50 tu ambapo baada ya kupanuliwa kwa sasa wana matanki mawili yenye jumla ya ujazo wa lita laki 1 na elfu 50.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa wazazi CCM Taifa Ndg.Gilbert Kalima akizungumza na wanachi hao amesema kuwa ni jukumu la wanaCCM kujadili na kuishauri Serikali kuwatatulia wananchi changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa kuwa CCM ndio imepewa ridhaa ya kuongoza nchi.
Aidha ameendelea kusema kuwa kila changamoto inayotolewa na wananchi wa eneo husika itawasilishwa kwenye kamati ya Halmashauri kuu CCM Taifa kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa utatuzi kwa lengo la kuwasaidia wananchi kupata maendeleo wanayoyahitaji.
Mradi huo wa maji ulianza kwa lengo la kutoa huduma katika vituo vya Afya na Zahanati kwa jili ya kupunguza shida ya mama wajawazito na waliojifungua kufuata maji umbali mrefu June 2019 ukifadhiliwa na AMREF,WATER AIDS na WEDECO.
Aidha Januari 29, 2020 mradi huo ulipanuliwa na RUWASA kwa kutumia Force Account chini ya usimamizi wa Ofisi ya RUWASA Mkoa , Wilaya pamoja na wananchi wa kijiji cha Lwamgasa ambapo ulikamilika Juni 2021 chanzo cha maji kikiwa ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita elfu 17 kwa saa kilichochimbwa kwa ufadhili wa WATER AIDS.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa