Katoro, Geita - Agosti 12, 2024
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameongoza mkutano wa hadhara katika viwanja vya CCM Katoro, Wilayani Geita, ambapo amesikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi. Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Dotto Biteko, na Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Nchemba.
Dkt. Nchimbi amepokea kero 108 kutoka kwa wananchi 61 na kutoa ufumbuzi wa kero hizo, huku baadhi zikikabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita,Mhe Martin Shigela, kwa hatua zaidi.
Balozi Dkt. Nchimbi Katibu Mkuu Chama cha Mapinduzi (CCM) amepokea kero 108 kutoka kwa wananchi 61 na kutoa ufumbuzi wa kero hizo, huku baadhi zikikabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita,Mhe Martin Shigela, kwa hatua zaidi.
Wabunge wa wilaya ya Geita , Mhe. Tumaini Magesa (Jimbo la Busanda) na Mhe. Joseph Musukuma (Jimbo la Geita vijijini), wamepongeza juhudi za Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kufanikisha miradi ya maendeleo, huku wakitoa wito wa kuundwa kwa Halmashauri ya Mamlaka ya mji mdogo wa Katoro kutokana na ongezeko la wakazi na shughuli za kiuchumi.
Mbunge wa Jimbo la Geita vijijini Mhe Joseph Musukuma ameeleza hofu ya wafanyabiashara kuhusu mamlaka ya mapato na kumuomba Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Katibu Mkuu kukaa na Mamlaka ya mapato Tanzania ( TRA) na wafanyabiashara kwani kuna tatizo
Kwa upande wake Mbunge Musukuma alieleza hofu ya wafanyabiashara kuhusu mamlaka ya mapato, akisema, "Nikuombe Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wakae TRA na wafanyabiashara kwani kuna tatizo, ni vyema mkutane na kujadili ili kufikia maelewano." Mbunge huyo pia alisisitiza umuhimu wa kutatua tatizo la gharama kubwa za mabango ya biashara katika mamlaka ya mji mdogo wa Katoro.
Wananchi Mkoa wa Geita wakiwa katika viwanja vya CCM-Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro walipofika kumsikiliza Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi katika mkutano wa hadhara Agosti 12,2024 ambapo kero mbalimbali zilitatuliwa.
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi alitangaza kuwa barabara ya Katoro kwenda Ushirombo yenye urefu wa kilomita 39 itaingia katika ujenzi wa kiwango cha lami mwaka huu, huku hatua za manunuzi na mazungumzo na mkandarasi zikiwa zimeanza. Pia, alibainisha kuwa barabara inayounganisha Geita na Shinyanga kupitia Mtakuja na Nyarugusu imeanza kutangazwa kwa mkandarasi ambapo zitasaidia shughuli za kiuchumi katika mikoa hiyo.
Katika jitihada za kuimarisha usalama, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe Daniel Bassil Sillo ametoa wito kwa mamlaka wa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi na kuahidi kujenga kituo cha polisi cha kisasa kwa mji wa Katoro. "Anzisheni vikundi vya ulinzi shirikishi na toeni taarifa kwa polisi ili kuchukua hatua. Msiwafuge wahalifu,"amesema Naibu Waziri.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, ameagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuitisha kikao cha wafanyabiashara wa Katoro ili kujadili kero zao na kuboresha mazingira ya biashara,huku Waziri wa fedha Dkt. Nchemba, akisisitiza kuwa serikali imechukua hatua madhubuti kushughulikia kero za kodi na wafanyabiashara. "Namuelekeza Meneja wa Mapato pamoja na wakurugenzi kushughulikia kero hizi. Rais ameunda kamati maalum kushughulikia mambo haya, na itaendelea kufanya kazi kuhakikisha mambo yanaenda vizuri," amesema Dkt. Nchemba.
Katika Mkutano huo Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dotto Biteko, amesifu mfumo wa kidigitali wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika ukusanyaji wa kero za wananchi, "CCM inafanya kazi yake kisayansi, Ukusanyaji wa kero kwa njia ya kidigitali unasaidia kufanya tathimini na kujua kero ngapi zimeshughulikiwa, na ni wangapi wamehusishwa. hatua hii ni muhimu katika utekelezaji wa ilani ya chama na kuimarisha uhai wa chama."amesema Mhe Biteko.
Viongozi mbalimbali wakihutubia katika mkutano wa Katibu Mkuu Chama cha Mapinduzi uliofanyika katika viwanja vya CCM-Katoro Agosti 12, 2024
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa