Kamati ya Mwenge wa Uhuru ya Mkoa wa Geita imefanya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayohusiana na maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, unaotarajiwa kupokelewa Oktoba 5, 2024, katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Ziara hiyo imefanyika leo, Septemba 10, 2024, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mwenge wa Mkoa ambaye pia ni Kaimu Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Geita, Eliphas Misenya. Kamati hiyo imeambatana na Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Alex Helman, pamoja na wataalamu kutoka ngazi ya mkoa na halmashauri.
Katika ziara hiyo, Kamati imetembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa sita katika Shule ya Sekondari ya Kasota. Kamati imefurahishwa na hatua iliyofikiwa, ikielezea matumaini makubwa ya kukamilika kwa mradi huo kwa wakati.
Mradi wa vyumba sita vya madarasa katika shule ya Sekondari Kasota.
Vilevile, Kamati hiyo imetembelea shamba la miti lililopo Kata ya Igate na kujiridhisha na matunzo bora ya shamba hilo, na kutoa pongezi kwa juhudi zinazofanywa kulihifadhi.
Mradi wa miti katika kata ya Igate.
Katika ziara ya Ofisi ya Kata ya Nzera, Mwenyekiti wa Kamati Eliphas Misenya amepongeza maendeleo ya ujenzi wa ofisi hiyo, akibainisha kuwa ushauri walioutoa awali umetekelezwa kwa ufanisi.
Mradi wa ujenzi wa ofisi ya kata ya Nzera, uliopo kata ya Nzera.
Kamati pia imetembelea ujenzi wa barabara ya lami nyepesi yenye urefu wa kilomita 1.1, ambayo inatarajiwa kuwekwa jiwe la msingi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru. Mhandisi wa TANROADS Mkoa wa Geita, Jonas Malugu, amepongeza hatua ya ujenzi wa barabara pamoja na maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Nzera, ambayo imefikia hatua za mwisho.
Mradi wa ujenzi wa Barabara ya lami nyepesi yenye urefu wa Kilomita 1.1 uliopo katika kata ya Nzera
Aidha, Kamati imekagua maendeleo ya kituo cha afya kilichoboreshwa kutoka Zahanati ya Nkome na sasa kikiwa na huduma za kina mama na watoto pamoja na jengo la maabara. Mganga mfawidhi wa Zahanati hiyo, Charles Kaflela, ameweka wazi kuwa kituo hicho kilichoboreshwa kitakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 3,000 kwa mwezi, ikilinganishwa na zaidi ya watu 1,800 waliokuwa wakihudumiwa hapo awali. Kituo hicho kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Oktoba 5, 2024.
Mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Nkome, kilichopo katika kata ya Nkome.
Kamati ya Mwenge wa Uhuru imeeleza kuridhishwa na maendeleo ya miradi iliyokaguliwa na kusisitiza umuhimu wa miradi hiyo kukamilika kwa wakati ili kutimiza malengo ya maendeleo katika Mkoa wa Geita.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa