Kamati ya fedha, uongozi na mipango Halmashauri ya Wilaya ya Geita Julai 17 imefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata mbalimbali za Halmashauri.
Makamu mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Isulwabutundwe Mhe.Maweda James Gwesandili na mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Rwamgasa Mhe. Kaparatusi Joseph na wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita wametembelea na kukagua utekelezaji wa miradi katika shule za Sekondari zilizopo katika kata za Ludete, Katoro na Nyarugusu.
Kamati ya fedha uongozi na mipango ikikagua ujenzi wa madarasa shule ya sekondari Bugayambelele kata ya ludete ambapo wamepongeza hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika mradi huo wenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni 214,400,000
Wakiwa kata ya Ludete kamati hiyo imetembelea miradi ya ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa na matundu 8 ya vyoo, iliyopo katika shule za sekondari Bugayambelele na Ludete, zenye zaidi ya wanafunzi 3000.
Kamati ya fedha uongozi na mipango ikikagua ujenzi wa matundu 8 ya vyoo katika shule ya Sekondari ya Ludete iliyopo katika kata ya ludete
Miradi hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 214,400,000 utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 97 ambapo Mhe Gwesandili amepongeza hatua iliyofikiwa katika ukamilishaji wa miradi hiyo.
Aidha katika shule ya Sekondari ya Ludete Mhe Gwesandili amepongeza ujenzi wa choo cha wasichana uliozingatia chumba cha kubadilishia taulo za kike pamoja na wanafunzi wenye ulemavu ambapo kamati hiyo imesisitiza miradi hiyo kuwa na mifumo bora ya maji kabla ya kukabidhiwa ifikapo Julai 30, 2024
Kamati ya fedha uongozi na mipango ikikagua ujenzi wa madarasa katika ziara iliyofanyika Julai 17. Kamati hiyo imewapongeza madiwani na watendaji wa kata pamoja na wakuu wa shule kwa usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa katika kata hizo
Kwa upande wa Kata ya Katoro kamati imetembelea mradi wa ukarabati wa vyumba vya maabara katika shule ya sekondari ya Samia. Mradi huo umegharimu shilingi Milioni 100 na unategemewa kutumika katika utafiti wa masomo ya Fizikia, Bailojia na Kemia ambapo utahudumia zaidi ya wanafunzi 500.
Ukamilishwaji wa Maabara kwa ajili ya kujifunzia masomo ya Sayansi (Fizikia, Bailojia na Kemia) katika shule ya Sekondari Samia wenye thamani ya shilingi Milioni 100 ambao utahudumia zaidi ya wanafunzi 500
Pia kamati imekagua mradi wa ujenzi wa vyumba 7 vya madarasa na ukamilishaji wa vyumba 4 vya madarasa katika shule ya Sekondari Lutozo ambao umekamilika kwa asilimia 98 huku thamani ya mradi ikiwa shilingi Milioni 224,637,700. Mradi huo utakapokamilika unaotarajia kuhudumia zaidi ya wanafunzi 2200
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Lutozo Mwl Revocatus Joseph Malaha ametoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha za miradi kiasi cha shilingi milioni 381 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa yatakayotumiwa na wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita unaotarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa kutembelea kata ya Nyarugusu na kukagua ujenzi wa bweni la wanafunzi wakike katika shule ya sekondari Evarist unaotekelezwa kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) pamoja na nguvu za wananchi wa kata hiyo. Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 180 na upo katika hatua ya boma.
Kamati hiyo imewapongeza madiwani na watendaji wa kata pamoja na wakuu wa shule kwa usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa katika kata hizo.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita inaendelea kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo ambayo inatekelezwa ndani ya Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa Mkurugenzi Mtendaji ndg Karia Rajabu Magaro.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Anuani ya Posta: S.L.P 139 Geita
Simu: +225 282520061
Mobile:
Barua pepe: info@geitadc.go.tz
Hakimiliki@ Halmashauri ya wilaya ya Geita , Haki zote zimehifadhiwa